1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kupambana na hisia za chuki dhidi ya Wayahudi

Oumilkheir Hamidou
4 Oktoba 2018

Kansela Angela Merkel yupo ziarani nchini Israel kwaajili ya kushiriki katika kikao cha saba cha mashauriano kati ya serikali ya Ujerumani na ile ya Israel. Kikao hicho kimeanza upya baada kusitishwa kwa muda mrefu.

https://p.dw.com/p/35zee
Israel Besuch Kanzlerin Merkel
Picha: Reuters/R. Zvulun

Akiwa ziarani nchini Israel kansela Angela Merkel ameshadidia "jukumu la Ujerumani katika kupambana na hisia za chuki dhidi ya Wayahudi.Ujerumani inalazimika daima kukumbuka," uhalifu usiokuwa na mfano uliofanywa na wazalendo wa kijamaa-NS dhidi ya wayahudi, hisia za chuki dhidi ya wayahudi, chuki dhidi ya wageni, chuki na matumizi ya nguvu" ameandika kansela Merkel katika daftari la kumbusho la wahanga wa mauwaji ya halaiki ya wayahudi huko Yad Vashem mjini Jerusalem.

Merkel atunukiwa shahada ya heshima ya uzamifu

Israel Besuch Kanzlerin Merkel
Kansela Merkel na shada la mauwa katiaka kumbukumbu ya Yad VashenPicha: Reuters/D. Hill

Akitunukiwa shahada ya heshima ya uzamifu katika chuo kikuu cha Haifa, kansela ameonyesha kushukuria kuona "maisha ya wayahudi yameanza kunawiri tena nchini Ujerumani."Maisha hayo ni sehemu ya kitambulisho cha Ujerumani amesema Kansela Merkel aliyeutaja urafiki pamoja na Israel kuwa ni zawadi adhimu.

Kansela Merkel na baraza lake la mawaziri walifika jana nchini Israel. Usiku  kansela Merkel aliandaliwa karamu maalum na waziri mkuu Benjamin Netanyahu .Katika kumbusho la Yad Vashen kansela Merkel aliweka shada la mauwa hii leo kuwakumbuka wayahudi milioni sita waliouliwa na wanazi katika vita vikuu vya pili vya dunia-Holocaust.

Kansela na msimamo wa Israel kuhusu Iran

Katika mahojiano pamoja na wanafunzi, mada kuu ilihusiana na hali ya kisiasa namna ilivyo katika eneo hilo.Kansela merkel ameonyesha kuuelewa msimamo mkali wa Israel kuelekea Iran.Anasema anaunga mkono msimamo wa Israel kudai "kila la kufanya lifanywe kuhakikisha Iran haimiliki silaha za nuklea.

Hitilafu za maoni lakini zinakutikana katika suala la makubaliano ya kimataifa ya mradi wa nuklea wa Iran .Kinyume na Israel,Ujerumani inaunga mkono makubaliano hayo.

Katika karamu ya chakula cha mchana leo pamoja na rais wa Israel, Reuven Rivlin, kansela Merkel amesema suala la usalama wa Israel "litaendelea kuwa mojawapo ya majukumu ya Ujerumani." Daima msimamo wa Ujerumani ni kuhakaikisha masilahi ya Israel yanatangulizwa mbele." amesema kansela Merkel.

Kitovu cha maashauriano kati ya serikali za nchi hizi mbili ambayo tangu miaka kumi iliyopita yamekuwa yakifanyika kila mwaka kati ya Ujerumani na Israel,kinahusiana na mada za kiuchumi, ubunifu na teknolojia. Katika mashauriano hayo leo jioni masuala yanayozusha mabishano yanatarajiwa kuzuka. Mbali na mradi wa nuklea wa Iran, mivutano inatarajiwa katika suala la ujenzi wa makaazi ya wayahudi katika ardhi za Wapalastina.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/KNA/AFP

Mhariri:Gakuba, Daniel