1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kutafuta kiti kisicho cha kudumu UN

Sylvia Mwehozi
28 Machi 2018

Waziri mpya wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas, anafanya ziara yake ya kwanza katika Umoja wa Mataifa leo Jumatano, katika jitihada za kuimarisha nafasi ya Berlin, kuchaguliwa katika kiti kisicho cha kudmu.

https://p.dw.com/p/2v7OE
UN Sicherheitsrat Abstimmung über Waffenruhe in Syrien
Picha: Getty Images/AFP/D. Emmert

Maas atajaribu kuwashawishi wajumbe wa Umoja wa Mataifa juu ya sifa ya Ujerumani, kwa ajili ya kiti kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa atakapowasili jijini New York. Hiyo ni ziara yake ya kwanza katika Umoja wa Mataifa na atahudhuria majadiliano ya ujumbe wa kulinda amani, pamoja na kukutana na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, mabalozi wenye ushawishi kutoka nchi kadhaa siku ya Jumatano ili kugusia sifa za Ujerumani kwa ajili ya kiti cha kutodumu kwenye baraza hilo.

"Tunataka kushirikshwa katika kukabiliana na changamoto kubwa za amani na usalama", alisema Maas kabla ya kuondoka mjini Berlin, akiongeza kwamba alitaka kuzungumza na wawakilishi wa nchi nyingine ili kusikia kile wanachotarajia kutoka kwa Ujerumani.

Ujerumani ni nchi ya nne mchangiaji mkubwa katika bajeti ya Umoja wa Mataifa na ya pili katika utoaji wa misaada ya kiutu na maendeleo. Jeshi la Ujerumani pia ni moja ya mchangiaji mkubwa wa magharibi katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani, ikiwemo nchini Mali. "Umoja wa Mataifa ni mhimili wa sheria za kimataifa ", akiongeza kwamba uhifadhi wake na maendeleo ni muhimu kwa maslahi ya Ujerumani.

Israel Jerusalem Heiko Maas trifft Benjamin Netanjahu
Heiko Maas akiwa na waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Imago/photothek/X. Heinl

Baraza la Usalama lenye wanachama 15 lina wajumbe watano wa kudumu wenye kura ya turufu, ambao ni Marekani, Urusi, China, Uingereza na Ufaransa na wengine 10 ambao si wanachama wa kudumu, wanaohudumu kwa kipindi cha miaka miwili na huchaguliwa na mkutano mkuu wa Umoja wa Umoja wa Mataifa.

Wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa watahudhuria mkutano wa Juni 8, ambapo Ujerumani, Ubelgiji na Israel zinawania nafasi ya viti viwili katika Ulaya magharibi na katika vipengele vya nchi nyingine.

Maas hata hivyo hatoitembelea Washington kama sehemu ya ziara yake ya kwanza tangu achukue wadhifa huo, alipochaguliwa katika serikali ya muungano ya Ujerumani mapema mwezi huu, na hiyo ni kwasababu waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson amebakisha muda mchache kabla ya kumaliza majukumu yake.

Badala yake ataitembelea Washington baada ya mrithi wa Tillerson, mkurugenzi wa shirika la ujasusi CIA,  Mike Pompeo atakapoanza rasmi kazi mwezi Aprili.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dw/dpa

Mhariri: Josephat Charo