1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kutoa msaada zaidi kwa Afrika?

Jane Nyingi
14 Novemba 2016

Mashirika mawili ya wataalamu Ujerumani yamewasilisha ripoti kwa Waziri wa Maendeleo Gerd Müller na kusema fedha zaidi zinahitajika kukabiliana na umaskini na kuimarisha uchumi wa bara la Afrika.

https://p.dw.com/p/2Sf08
Kiwanda cha maharage Msumbiji
Picha: DW/M. David

Kwa mujibu wa mashirika hayo iwapo Ujerumani haitachukulia kwa makini ripoti hiyo upo uwezekano wa kuongezeka  idadi ya wahamiaji kutoka Afrika wanaohatarisha maisha yao ili mradi tu wafike Bara Ulaya. Mapendekezo hayo ni pamoja na Ujerumani kuanzisha hazina ya siku za baadae ambayo mwanzoni  itakuwa na Euro billion 120 kutoka kwa wawekezaji binafsi.

Fedha hizo zitatumika  katika sekta ya nishati mbadala, maendeleo ya viwanda na kuboresha miundo mbinu. Kwa sasa Ujerumani inatumia Euro mbili kwa kila mtu Afrika katika maswala ya maendeleo, kiasi hicho cha hela ni kidogo sana. Wataalamu hao pia wameonya  kuwa idadi ya wahamiaji kutoka Afrika itaongezeka kwa kasi katika siku zijazo iwapo hakuna hatua zitakazokuwa zimepigwa katika kuunda nafasi za ajira kwa vijana wa bara hilo.

Waziri huyo wa maendeleo wa hapa Ujerumani Gerd Müller anaunga mkono wazo hilo na kusema  katika kipindi cha wiki kadhaa kijacho atawasilisha wao lake kama hilo. "Ni lazima tuwekeze katika nchi hizo, tunahitaji kuwapa watu matumaini. Vinginevyo hatutashuhudia mamia kwa maelfu ya wakimbizi bali mamilioni  katika miungo kadhaa ijayo. Kwa hivyo vijana Bara Afrika hatakuwa bila ajira na kutofahamu hali yao ya baadae katika nchi zao,” amesema Müller.

Wakimbizi watakiwa kusaidiwa zaidi

Waziri wa ushirikiano wa kimaendeleo Ujerumani, Gerd Mülle
Waziri wa ushirikiano wa kimaendeleo Ujerumani, Gerd MüllerPicha: picture-alliance/Sebastian Gol

Uchunguzi wa mashirika hayo pia ulibaini kuwa Afrika ina uwezo mkubwa katika maeneo kama vile kilimo na nishati mbadala. Kufuatia hilo wanapendekeza  ujenzi wa vituo vya uzalishaji nishati inayotokana na jua  katika baadhi ya maeneo ya Bara la Afrika, ambavyo havitatoa tu nafasi za ajira  lakini pia  kutatoa tatizo sugu la ukosefu wa nguvu za umeme katika bara hilo swala alilokubaliana nalo Waziri Müller. "Ni kuhusu  kuimarisha  na kuendeleza uwezo  wa watu wao wenyewe. Sio eti twende kule na mipango yetu  na fedha zetu  na pia tushiriki katika usimamizi. Sisi hatutaki ukoloni mambo leo. Hivyo ndivyo inavyofanya China. Huo sio mtizamo wetu."

Ripoti hiyo pia inatoa wito wa kupanuliwa programu ya misaada ya kiutu kwa wakimbizi na pia wakimbizi wa ndani kwa ndani. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wakati wa ziara yake nchini Niger hata hivyo aliondoa uwezekano wowote wa Ujerumani kutenga mfuko wa fedha kwa maendeleo Barani Afrika. Kansela Merkel alisema hali ilivyo hivi sasa Afrika ni tofauti na ilivyokuwa bara ulaya wakati wa vita vya pili vya dunia. Mpango huo uliopendekezwa na mashirika hayo ni sawia na ule uliotolewa na Marekani kwa Bara Ulaya ili kujijenga upya kufuatia vita vya pili vya dunia.

Mwandishi: Jane Nyingi/Africa Link

Mhariri: Yusuf Saumu