1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Nchi tatu Afrika ni salama kurejeshwa wakimbizi

Bruce Amani
18 Julai 2018

Baraza la mawaziri la Ujerumani limekubali kuziorodhesha nchi tatu za kaskazini mwa Afrika pamoja na Georgia kama nchi zilizo salama ili kuharakisha mchakato wa kuwapatia hifadhi wahamiaji 

https://p.dw.com/p/31hc3
Deutschland - Kabinettssitzung in Berlin
Picha: Getty Imagas/AFP/J. MacDougall

Baraza la mawaziri limekubaliana leo na rasimu inayoziorodhesha Morocco, Tunisia , Algeria na Georgia kuwa nchi salama.  Rasimu hiyo sasa itapaswa  kupigiwa kura na bunge la Ujerumani - Bundestag.

Jaribio la awali la kuziorodhesha nchi hizo pekee tatu za Afrika Kaskazini lilishindwa katika baraza la --- Bundesraat katika kipindi cha mwisho cha bunge. Wapinzani wa chama cha Kijanmi na chama cha siasa kali za kushoto cha Die Linke tayari vimeukataa mpango huo, wakisema kuwa nchi hizo sio salama kwa makundi fulani.

Waziri wa Mambo ya Ndani Horst Seehofer ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Bavaria cha CSU ambacho ni ndugu na chama cha Kansela Angela Merkel cha CDU, aliipongeza hatua hiyo iliyofikiwa na serikali. "Huu ni mchango mwingine muhimu kwa lengo letu la kisiasa kwamba tunataka ubinaadamu kwa upande mmoja, kwa kuruhusu haki ya hifadhi. Kwa upande mwingine, pia tunataka kuweka utaratibu katika kushughulikiwa watu ambao hawawezi kukata rufaa dhidi ya haki hii ya hifadhi. Ndio maana nina furaha kuwa ufafanuzi huu umewekwa katika mswada huu".

Pressekonferenz mit Horst Seehofer
Waziri wa mambo ya ndani Horst SeehoferPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Kundi la kutetea haki za waomba hifadhi la Pro Asyl limesema rasimu hiyo mpya ya sheria itajumuisha kipengele cha kuwaruhusu wale ambao wameanza kazi, mafunzo ya kitaaluma au mafunzo ya kazi kabla ya tareje ya leo, kubakia Ujerumani.

Kawaida, waomba hifadhi au wale wanaopewa kibali cha kubaki kutoka nchi ambazo ni salama huwa hawaruhusiwi kufanya kazi Ujerumani.

Kundi la Pro Asyl linapinga rasimu ya sheria hiyo ya serikali, likisema suala la utaratibu wa kuharakishwa bila kuzingatia ushahidi wa hali ya muomba hifadhi binafsi halijatambuliwa kikamilifu.

Robert Habeck, kiongozi wa chama cha Kijani, amesema leo kuwa nchi hizo tatu za Afrika Kaskazini, ambazo ni sehemu ya eneo la Maghreb, sio salama kwa watu wengi.

Habeck ameliambia shirika la habari la RedaktionsNetzwerk Deutschland kuwa bado wanahabari, makundi ya walio wachache na mashoga hawako salama dhidi ya mateso na kukamatwa katika mataifa ya eneo la Maghreb.

Mwanasiasa huyo ameongeza kuwa kuorodheshwa kwa nchi hizo kuwa salama hakusuluhishi matatizo yoyote ambayo hatua hiyo inalenga. Anasema kama suala ni kuwarejesha watu katika nchi zao haraka, unahitaji kuwa na makubaliano yanayofanya kazi ya kuwahamisha watu. Na kama suala ni kukabiliana na uhalifu nchini Ujerumani, basi unahitaji jeshi la polisi lenye uwezo wa kutosha.

Mbali na nchi zote za Umoja wa Ulaya, nchi nyingine ambazo ni salama kwa mujibu wa serikali ya Ujerumani ni: Ghana, Senegal, Bosnia-Herzgovina, Macedonia, Serbia, Montenegro, Albania na Kosovo.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Iddi Ssessanga