1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Vifo kutokana na mafuriko vyapindukia watu 140

Zainab Aziz Mhariri:Saumu Njama
18 Julai 2021

Vifo vinazidi kuongezeka wakati Ujerumani ikitafakari uharibifu uliosababishwa na mafuriko. Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier awatembelea waathiriwa wa mafuriko.

https://p.dw.com/p/3wdX3
Deutschland Unwetter Steinmeier und Laschet in Erftstadt
Picha: Staatskanzlei NRW/dpa/picture alliance

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, ametembelea jimbo la North Rhine-Westphalia ambalo limeathirika zaidi na mafuriko. Steinmeier alionekana ni mwenye majonzi alisema anaomboleza pamoja na waliopoteza ndugu au marafiki. Amesema masaibu yaliyowafika familia hizo yamewavunja moyo wajerumani.

Steinmeier amesema baada ya mkutano na waokoaji katika mji wa Erftstadt kwamba watu wengi wamepoteza kila kitu walichokuwa nacho kwenye maisha yao kama mali zao na nyumba zao na vitu vingine vingi.

Wanajeshi wakishughulikia athari za mafuriko katika mji wa Erftstadt
Wanajeshi wakishughulikia athari za mafuriko katika mji wa ErftstadtPicha: David Young/dpa/picture alliance

Zaidi ya watu 140 wamekufa katika eneo la magharibi mwa Ujerumani huku vifo zaidi vikiripotiwa barani Ulaya kote.Watu wengine 670 wamejeruhiwa katika mafuriko hayo.Taarifa ya polisi imesema watu wengi bado hawajulikani walipo.

Serikali ya Ujerumani imewapeleka wanajeshi 850 kusaidia katika maafa hayo yaliyotokea. Rais Frank-Walter Steinmeier alitembelea maeneo yaliyoathirika zaidi na mafuriko ya North Rhine - Westphalia.

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier
Rais wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Kansela Angela Merkel atatembelea maeneo yaliyokumbwa na mafuriko nchini Ujerumani leo Jumapili ili kujionea uharibifu na pia kukutana na waathiriwa, baada ya siku kadhaa za mvua kubwa zilizonyesha katika maeneo ya Ulaya magharibi.

Bibi Merkel atakwenda katika kijiji cha Schuld katika jimbo la Rhineland-Palatinate, mojawapo ya maeneo mawili yaliyoathirika zaidi magharibi mwa Ujerumani, ambapo mto wa Ahr uliofurika uliharibu nyumba na kuacha vifusi cikiwa vimejaa katika mitaa ya mji huo.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

Mkoa wa Upper Bavaria, ambao uko katika jimbo la kusini mwa Ujerumani la Bavaria, pia unashuhudia hali za dharura. Wazima moto wamepelekwa katika eneo hilo kukabiliana na barabara zilizojaa maji na maporomoko ya ardhi katika mkoa huo.

Wakati ambapo maji ya mafuriko yanaendelea kupungua sehemu nyingi zilizoathiriwa zimeweza kufikiwa na hivyo kujionea kiwango cha uharibifu kilichotokea.

Waziri wa Fedha wa Ujerumani Olaf Scholz, pamoja na Waziri wa Uchumi Peter Altmaier, wameahidi msaada kwa wahanga wa mafuriko hayo.

Waziri wa Fedha wa Ujerumani Olaf Scholz
Waziri wa Fedha wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Luca Bruno/AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo kiongozi wa Chama cha Kijani Robert Habeck ametoa wito wa kutolewa msaada wa haraka kwa waathiriwa, amesisitiza juhudi za pamoja na za ulinzi zaidi kuwekwa ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Maeneo mengine yaliyoathirika pia ni ya karibu na mipaka kati ya Ujerumani na nchi za Ubelgiji, Uholanzi na Luxembourg. Mafuriko hayo pia yameathiri sehemu ya mashariki mwa Ujerumani na nchi jirani ya Austria.

Bwawa la Steinbachtal lawatia wasiwasi maafisa

Ijapokuwa mafuriko yamepungua katika maeneo mengi, wakaazi walio katika mji wa Euskirchen, eneo mojawapo ya jiji kuu la Cologne wamo kwenye hatari ambapo bwawa la Steinbachtal linaweza kufurika wakati wowote. 

Kina cha maji chaongezeka kwenye mito
Kina cha maji chaongezeka kwenye mitoPicha: Christoph Hardt/Future Image/imago images

Bwawa hilo halijatulia kabisa baada ya sehemu kubwa kupasuka kutokana na maji mengi. Mamlaka ya jiji la Cologne imesema inahofia hatari kubwa ya mafuriko katika maeneo yaliyo chini ya bwawa hilo lakini mipango imewekwa ya kuwahamisha watu kutoka kwenye eneo hilo.

Huku mvua zilizonyesha barani Ulaya zikiwa zimeleta maafa makubwa, ujenzi utakaogharimu mamilioni ya Euro unasubiriwa kuanza.

Vyanzo:/AFP/AP/https://p.dw.com/p/3wbW7