1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaiangamiza San Marino

Bruce Amani
11 Juni 2017

Sandro Wagner alifunga mabao matatu katika mechi yake ya pili akiwa na timu ya taifa ya Ujerumani wakati mabingwa hao watetezi wakiendeleza rekodi yao bora katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia kwa kuizaba San Marino 7-0

https://p.dw.com/p/2eT7U
Fußball WM-Qualifikation Deutschland - San Marino Torjubel
Picha: Reuters/M. Rehle Livepic

Ujerumani ilifunga mabao 27 katika mechi tatu za awali dhidi ya taifa hilo dogo, na suali lilikuwa tu ni mabao mangapi ambayo timu hiyo mpya ya Ujerumani ingeweza kufunga mara hii.

Mwishowe, ulikuwa ushindi mkubwa kabisa wa Ujerumani nyumbani chini ya kocha Joachim Loew.

Kikosi cha kwanza cha Ujerumani kiliundwa kutoka vilabu 11 tofauti kwa mara ya kwanza katika miaka 57 wakati Loew aliipa timu yake ya majaribio itakayocheza katika dimba la Kombe la Mashirikisho nafasi ya kuyanoa makali.

"unaweza kujaribu vitu kadhaa katika mechi hizi, kupata uzeofu, kujiamini na kuonyesha mchezo mzuri. Nimeridhika na hilo”. Alisema Loew. "Sio kila kitu kilikuwa shwari lakini mambo kadhaa yalifauliu”. Aliongeza.

Mabao mengine ya mchuano huo yalifungwa na Julian Draxler, Amin Younes, Mustafi na Julian Brandt

Fußball WM-Qualifikation Deutschland - San Marino Torjubel Sandro Wagner
Wagner alikuwa mwiba katika safu ya mashambuliziPicha: Reuters/M. Rehle Livepic

Ujerumani sasa imeshinda mechi sita kati ya sita, na kufunga mabao 27 huku wakifungwa moja pekee katika Kundi C na inalenga kukamilisha shughuli ya kufuzu mapema iwezekanavyo. Hatua ya kuwapumzisha karibu wachezaji wake wote wa kawaida haikuwa na tofauti yoyote kwenye mchezo wa jana.

Washindi wa kila kundi kutoka makundi tisa watafuzu moja kwa moja katika dimba la Kombe la Dunia la Urusi litakalozishirikisha timu 32. Timu nane zitakazomaliza katika nafasi ya pili kwenye kila kundi zikiwa na rekodi bora dhidi ya timu za kwanza, tatu, nne na tano katika makundi yao zitaingia mechi za mchujo ili kuamua atakayetinga katika nafasi nyingine nne za dimba hilo zilizotengewa bara Ulaya.

Katika matokeo mengine ya Kundi C

NORWAY 1, JAMHURI YA CZECH 1

Theodor Gebre Selassie alifunga dakika kumi kabla ya kipindi cha kwanza kukamilika, lakini Alexander Soderlund wa Norway akasawazisha  kupitia mkwaju wa penalti wakati Jamhuri ya Czech ikishuka chini na pengo la pointi nne nyuma ya Ireland Kaskazini

AZERBAIJAN 0, IRELAND KASKAKAZINI 1

Bao la dakika za majeruhi la Stuart Dallas lilihakikisha kuwa Ireland Kaskazini ilijiimarisha katika nafasi ya pili ya kundi hilo, pointi tano nyuma ya Ujerumani, na kuendelea kuyauwa matumaini ya Azerbaijan kupata nafasi ya kucheza mechi za mchujo.  Azerbaijan ilisalia katika nafasi ya nne na pointi saba, ambapo sasa iko nyuma ya Ireland Kaskazini na pengo la pointi sita.

Mwandishi: Bruce Amani/APE
Mhariri: Sekione Kitojo