1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaingia katika Baraza la Usalama.

Abdu Said Mtullya12 Oktoba 2010

Ujerumani imefanikiwa kuchaguliwa kuwa mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/Pctj
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.Picha: picture alliance/dpa

Ujerumani imefanikiwa kupata kiti kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ujerumani itaanza kukikalia kiti hicho mwaka ujao japo siyo cha kudumu.Kiti hicho ni heshima kubwa kwa Ujerumani japo itakikalia kwa muda wa miaka miwili.

Kufanikiwa kwa Ujerumani kuchaguliwa kuwa mwanachama wa muda wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kunatokana na kampeni kubwa aliyoifanya waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Guido Westerwelle aliekuwa na matumaini ya kufanikiwa kutokana na sifa ya Ujerumani duniani.

Hapo awali kabla kura kupigwa balozi wa Ujerumani nchini Marekani Jürgen Chrobog alisema japo siyo lazima kwa Ujerumani kuwamo katika Baraza la Usalama,lakini ni jambo la heshima.

Pamoja na wanachama watano wa kudumu kwenye Baraza hilo Ujerumani itaungana na India,Afrika Kusini na Colombia katika kulitumikia baraza hilo kwa kuiwakilisha kanda ya Ulaya.Canada pia ilikuwamo katika kinyang'anyrio cha kugombea kiti lakini iliamua kujitoa na kuiwezesha Ureno kuingia katika Baraza la Usalama.Canada ilijitoa baada ya raundi ya pili kwenye Baraza Kuu ambapo Ureno ilikuwa mbele kwa kura 120 wakati Canada ikiwa na kura 78.

Ujerumani ilifanikiwa kupita katika raundi ya kwanza. Baada ya kura ya siri kupigwa katika raundi hiyo ,Ujerumani tayari ilifanikiwa kupata theluthi 2 ya kura

Katibu Mkuu wa chama cha waliberali FDP , Christian Lindner amesema kuwa leo ni siku nzuri kwa Ujerumani.Bwana Lindner amesema kuchaguliwa kwa Ujerumani kuwa mwanachama wa Baraza la Usalama kunaipa nchi hiyo fursa kubwa katika kushiriki katika utekelezaji wa majukumu ya kimataifa na kushiriki katika juhudi zinazofanywa na jumuiya ya kimataifa kwa lengo la kupunguaza silaha. Katibu Mkuu huyo wa chama cha FDP amesema kuchaguliwa Ujerumani kuwa mwanachama wa Baraza la Usalama baada ya miaka 20 tokea Ujerumani iungane tena ni ushuhuda wa imani ya jumuiya ya kimataifa juu ya Ujerumani.

Mwandishi/Mtullya abdu/DPA/ RTRE/

Mhariri/Josephat Charo/