1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yamtunukia tuzo Madonsela

Jane Nyingi
23 Novemba 2016

Mama Thulisile Madonsela kutoka Afrika ya Kusini hii leo anatunukiwa tuzo ya Ujerumani kwa bara la Afrika ya mwaka 2016 katika halfa itakayofanyika mjini Berlin hapa Ujerumani kutokana na kupambana na rushwa.

https://p.dw.com/p/2T6kF
Südafrika Thuli Madonsela
Picha: Getty Images/AFP/S. Heunis

Mama huyo amepata umaarufu kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya rushwa  alipokuwa anahudumu kama mlinzi wa maslahi ya umma nchini humo. Kashfa alizofichua Madonsela zimemhusisha hata Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma.Huku raia wengi wa Afrika kusini wakiendelea kuishi katika lindi la umaskini, wanasiasa wanaochukuliwa kuwa wala rushwa wameendelea kujijengea utajiri. Rais Jacob Zuma ni miongoni mwa waliohusishwa na kashfa kadhaa ikiwemo ile ambapo fedha za walipa kodi zilitumika kukarabati makaazi yake binafsi. Aliyefichua kashfa hiyo ni Thulisile Madonsela wakati huo akiwa anahudumu kama mlinzi wa maslahi ya umma.

Katika mahojiano ya kipekee na runinga ya DW mjini Berlin, Thuli kama anavyofahamika na Waafrika kusini wengi alisema halikuwa jambo rahisi hasa kufichua kashfa hiyo ya rais Zuma kwani alipokea vitisho vingi. "Rais Zuma amekuwa akipokea vizuri matokeo mengi ya uchunguzi, lakini bila shaka mara mbili matokeo yaliyomuhusu, hakuyashughulikia kama nilivyotarajia. Nilipokea vitisho kutokana na hilo si moja kwa moja kutoka kwa rais au serikali bali washirika wake ambao walinitaka kuzifutilia mbali kesi kuhusu kashfa hizo au nifanye uchunguzi wa kina, lakini hakukuwepo na msingi wa kufanyika uchunguzi wa kina kuliko tulivyokuwa tumeagizwa kufanya."

Südafrika Präsident Jacob Zuma
Rais Jacob ZumaPicha: Imago/Gallo Images

Pamoja na wafanyakazi wake 300 mlinzi huyo wa maslahi ya umma alipokea malalamiko ya raia wa kawaida ambao hawakuwa na uwezo wa kuwa mawakili. Takriban malalamiko 40,000 yameshugulikiwa na bi Madonsela alipokuwa ofisini kwa miaka saba na kati ya malalamiko hayo elfu 30 yalifanikiwa. Rais Zuma alipomchagua  mwaka 2009 alimtaka ahakikishe kuwa ofisi yake inakuwa wazi kwa raia wote na kwamba atafanya kazi zake bila upendeleo wala woga. Na tangu kupewa wadhfa huo Madonsela alifanya kazi bila kuchoka na alidai wakati wote haki kutoka pande zote za watu wenye uwezo na wasio nao. Na anasema hakikuwa kibarua rahisi."Ilikuwa mara nyingi ni vigumu kwa watu kuelewa kuwa tunaweza kumuagiza afisa yeyote mkuu wa serikali kufanya kitu na bila shaka  kwa heshima."

Südafrika Tausende protestieren vor Präsidentenpalast gegen Zuma
Maandamano ya kumtaka rais Zuma kuondoka madarakaniPicha: Reuters/M. Hutchings

Tuzo hiyo anayoipokea Thuli Mandonsela hutolewa kwa mtu aliyetimiza vigezo vinavyohimiza uhuru, demokrasia na haki za binadamu. Waafrika Kusini sasa wanamtaka kujitosa katika siasa ili kuwatetea wanyonge wito aliokataa mama huyo aliyezaliwa na kulelewa mtaa wa mabanda wa Soweto.

Mwandishi:Jane Nyingi/Afrika link
Mhariri:Josephat Charo