1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaomboleza kifo cha kipa Robert Enke

16 Novemba 2009

Kamerun na Nigeria zakata tiketi zao za Kombe la dunia 2010.

https://p.dw.com/p/KYQZ
Teresa, kizuka marehemu R.Enke (kushoto)Picha: AP

KOMBE LA DUNIA KANDA YA AFRIKA:

Simba wa nyika -Kamerun na Super Eagles-Nigeria ,zilizifuata jana Ghana na Ivory Coast katika Kombe lijalo la dunia nchini Afrika kusini-kanda ya Afrika.

Mabingwa wa Afrika Misri, walihitaji bao la dakika za mwisho kuweka miadi ya mwisho na Algeria Jumatano hii mjini Khartoum,Sudan kuamua nani kanda ya Afrika, anatoroka na tiketi ya mwisho ya Kombe la dunia.Ujerumani nzima yaomboleza kifo cha kipa wa Taifa, Robert Enke.

Nigeria na Kamerun, zinarudi katika kombe la dunia baada ya kupigwa kumbo nje ya kombe lililopita nchini Ujerumani 2006.

Nigeria ilikata tiketi yake mjini Nairobi, Jumamosi kufuatia mabao maridadi ya jogoo la Bundesliga Obafami Martin ,alielifumania lango la Harambee Stars mara 2.Kwa ushindi wa mabao 3-2,Super eagles, inarudi katika kombe la dunia kama Ghana,Ivory Coast na wenyeji Afrika Kusini.

Wakati usalama mkali ulitanda mjini Cairo, kabla na baada ya mpambano kati ya Misri na Algeria, ilikua shangwe na shamra shamra mjini Lagos ,Nigeria na Yaounde ,Kamerun. Tunisia imepigwa kumbo na machinga Msumbiji mjini Maputo baada ya kulazwa kwa bao 1:0.

Simba wa nyika Kamerun wanarudi kunguruma katika msitu wa dimba la Afrika, kwani, wanadai Kombe la dunia barani Afrika bila ya simba wa nyika, haiwezekani.Kwa mabao 2:0 dhidi ya Simba wa Atlas,Morocco, Kamerun ikitamba na jogoo lake Samuel Eto'o ,ilitoroka na tiketi yake ya sita ya Kombe la dunia tangu kutamba pamoja na Algeria ,1982 huko Spain.

Simba wa nyika, waliingia uwanjani wakiongoza kwa pointi 1 zaidi katika kundi lao kuliko mahasimu wao wa karibu kabisa Gabon na kwa kuipiga kumbo Morocco, imeparamia kileleni mwa kundi A ikiwa na pointi 4 zaidi kuliko Gabon ililazwa kwa bao 1:0 na Togo.Simba wa nyika walikata tiketi yao ya Afrika kusini masaa machache tu baada ya Nigeria kuitimua nje Harambee Stars-Kenya na kuparamia kileleni mwa kundi B na kujiunga na wenyeji Afrika Kusini, Ghana na Tembo wa Ivory Coast.

Macho sasa yanakodolewa changamoto ya kufa-kupona baina ya majirani 2 na mahasimu wakubwa wa dimba-(mafiraouni) Misri na Algeria mjini Khartoum. Wapi tiketi ya mwisho ya kanda ya Afrika itaelekea ni vigumu kuagua.

Mashabiki wenye jazba kubwa ya dimba walizikaribisha timu hizo mbili zilipowasili jana Khartoum kwa changamoto yao ya Jumatano hii.Baada ya Misri kusawazisha dakika ya mwisho ya kufidia hapo Jumamosi usiku, Misri na Algeria ,zimebidi kupambana kwa mara ya 3 kuamua hatima yao.Mamia ya wafanyikazi wa Misri nchini Sudan, watazamiwa kuishangiria timu yao .swali je, mpambano huu utamalizika salama ?

Kwani, hamasa na jazba za mashabiki wa pande hizi mbili ni kubwa.Kufuatia kupigwa mawe kwa basi la timu ya Algeria,ilipowasili kwa mpambano wa jumamosi, machafuko yalizuka Marseille, Ufaransa usiku wa Jumamosi .Mashabiki wa Algeria walivunja madirisha ya maduka , waliwrushia polisi mawe na wakazitia moto marekebu kadhaa zilizoegesha katikabandari ya Marseille wakuchukizwa na ushindi wa juzi wa mabao 2 ya misri.Si chini ya boti 6 ziliharibiwa.Polisi wamearifu kwamba ghasia zilianza baada ya vijana wa asili ya kialgeria walipochukizwa na bao la dakika ya mwisho za kufidia la Misri.Jumatano hii basi ,itakua "asie na mwana aeleke jiwe na asie na mguu atie gongo-mkutano Khartoum,Sudan" ,upande wapili wa mpaka na Misri.

Mwishoe, takriban Ujerumani nzima, jana iliomboleza kifo cha kipa wa taifa wa Ujerumani ,Robert Enke.Umati ulikuwa uwanjani mjini Hannover,mitaani na wasioweza walihuzunika mbele ya TV majumbani.

Rais wa Shirikisho la dimba la Ujerumani,Thoeo Zwanzinger, aliwazindua mashabiki na wachezaji mpira: "mpira sio kila kitu.Usiwe ndio thamani pakee ya maisha ya mwanadamu. Timu nzima ya Taifa ya Ujerumani, ikiongozwa na nahodha Michael Ballack ilikuwa uwanjani kumuaga mwenzao.

Jumamosi ijayo, Bundesliga itaanza upya -ikiwa imejifunza darasa jipya-mpira sio kila kitu.Hannover ina miadi na Schalke kuania pointi 3.Langoni lakini, hatakuwapo Robert Enke upande wa Hannover.

Mwandishi:Ramadhan Ali/ AFPE/ERTE

Uhariri:Abdul-Rahman