1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yasikitishwa na mauaji ya Gaza

John Juma
1 Machi 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, ameelezea kushitushwa kwake na mauaji yaliyofanyika Gaza siku ya Alhamis wakati misaada ya kibinaadamu ilipokuwa ikitolewa na ameitaka Israel kufafanua yaliyojiri.

https://p.dw.com/p/4d5EV
Annalena Baerbock
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock.Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Kwenye ukurasa wake wa X, Baerbock aliandika siku ya Ijumaa (Machi 1) kuwa ameshtushwa akieleza kuwa watu walitaka misaada na kwa familia zao lakini baadhi wakafa.

Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, ambayo ni miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa Israel, alisisitiza kuwa jeshi la Israel ni sharti lichunguze kikamilifu hofu kubwa na ufyatuliaji risasi uliotokea.

Soma zaidi: Watu 104 wauwawa katika operesheni ya kutoa msaada Gaza

Wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas ilisema zaidi ya watu 100 waliokuwa kwenye foleni yakupokea misaada waliuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel.

Lakini jeshi la Israel limekanusha madai hayo na kusema vifo hivyo vilitokana na mkanyagano.

Mataifa kadhaa yameilaani Israel kwa mkasa huo, zikiwemo India, China, Uturuki, Saudi Arabia, Misri na Jordan.

Wizara ya afya ya ukanda huo imesema idadi ya vifo tangu vita vilipoanza Oktoba 7, imepindukia 30,000.