1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yawakumbuka wahanga wa shambulizi la Solingen

Bruce Amani
29 Mei 2018

Ujerumani leo inawakumbuka wahanga watano wenye asili ya Kituruki waliochomwa moto kwenye nyumba yao miaka 25 iliyopita. Shambulizi hilo la kibaguzi lilifanywa katika mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Solingen

https://p.dw.com/p/2yUl2
25 Jahre nach Solinger Brandanschlag
Picha: dpa

linakumbusha namna wanasiasa wanavyopaswa na wasivyopaswa kushughulikia ongezeko la matukio ya kibaguzi na chuki dhidi ya wageni. Mwandishi wa DW Fürstenau, Marcel ameandika ripoti ifuatayo, inayosomwa studioni na Bruce Amani))

Mnamo Mei 29 1993, kikundi cha watu wanaowachukia wageni kiliichoma moto nyumba moja mjini Solingen magharibi mwa Ujerumani. Wanawake watano wa Kituruki wakiwemo wasichana wadogo waliuawa. Saime Genc ndiye alikuwa mhanga mdogo kabisa akiwa na umri wa miaka minne. Wahanga wengine walikuwa Hülya Genc umri wa miaka 9, Gülüstan Öztük miaka 12, Hatice Genc miaka 18 na Gürsün Ince miaka 27.

Waliohusika walitambuliwa kuwa kikundi cha vijana wa kati ya umri wa miaka 16 na 23. Walikuwa wanachama wa kundi moja la siasa kali za mrengo wa kulia mjini Solingen. Katika mwaka wa 1995, walihukumiwa kifungo cha miaka 10 hadi 15 gerezani kwa mashitaka matano ya mauaji, 14 ya kujaribu kuuwa na kuchoma moto.

Deutschland Jahrestag 25 Jahre Solinger Brandanschlag | Mevlüde Genc, Angehörige von Opfern
Mevlüde Genc, alinusurika shambulizi hiloPicha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Sheria za hifadhi ziliimarishwa

Wakati hakuna uhusiano wowote wa wazi, ni vyema kujua kuwa shambulizi hilo la Solingen lilifanyika siku tatu tu baada ya bunge la Ujerumani – Bundestag kuchukua hatua kali ya kudhibiti haki ya kupewa hifadhi. Serikali ya muungano iliyovihusisha vyama vya Christian Democratic Union – CDU; Christian Social Union – CSU na Free Democrats FDP, ikiungwa mkono na chama cha upinzani cha Social Democratic – SPD, iliidhinisha marekebisho kwenye katiba ya Ujerumani.

Kwa miaka mingi, idadi ya kila mwaka ya waomba hifadhi ilibaki chini ya 100,000. Lakini mwaka wa 1990, kukawa na karibu maombi 200,000 na miaka miwili baadaye, idadi hiyo ikaongezeka mara mbili hadi 438, 191.

Hisia zilikuwa za ‘sumu'

Katika miaka ya 1990, kauli mbiu ya "Wageni nje” ilidhihirisha hisia za chuki zilizotanda katika baadhi ya miji ya Ujerumani. Sababu kadhaa zilichangia hali hiyo ya ubaguzi.

Katika iliyokuwa Ujerumani Mashariki, uchumi ambao awali ulidhibitiwa na serikali uliporomoka baada ya kuungana kwa Ujerumani mbili. Mamilioni ya Wajerumani wa Mashariki wakakosa kazi au kujihisi kuwa raia wa daraja la pili kutokana na sababu nyingine. Kwa wale waliotafuta kisingizio, "wageni” ndio waliolengwa kwa urahisi.

Deutschland Brandanschlag in Solingen
Waturuki watano wa familia moja walichomwa motoPicha: Imago/Tillmann Pressephotos

Ujerumani Mashariki ilikuwa na raia wachache wa kigeni kuliko iliyokuwa Ujerumani Magharibi. Hatahivyo, hali hiyo ya kuvunjwa moyo Magharibi mwa Ujerumani baada ya kuungana Ujerumani ilielekezwa kwenye makundi mengine ya walio wachache.

Anetta Kahane, mkuu wa shirika linalopinga ubaguzi lenye makao yake mjini Berlin la Wakfu wa Amadeu Antonio, anasema ni rahisi kulinganisha kati ya hisia kali za miaka 25 iliyopita na hali ya sasa

Mazingira ya kijamii yaliyotokana na hali hiyo pia yalisababisha kifo cha mtu mwenye jina linalofanana na Wakfu anaoongoza. Amadeu Antonio, aliyekuwa na asili ya Angola, alipigwa hadi kufa katika eneo la Eberswalde karibu na Berlin mnamo Novemba 1990 na kikundi cha vijana wa siasa kali za mrengo wa kulia. Watano kati ya washambuliaji hao watano walifungwa miaka minne jela huku wengine wakipewa vifungo vya nje.

Kahane anawatuhumu waliokuwa kwenye siasa katika wakati wa wimbi la mashabulizi ambayo yalikuwa na aina Fulani ya picha iliyokuwa na athari mbaya kabisa kuhusu namna wahamiaji walivyotendewa.

Anasema wanasiasa na maafisa walizijibu hisia za chuki dhidi ya wahamiaji kwa kupunguza idadi ya wale walioruhusiwa kuingia Ujerumani na hivyo kutuma "ishara mbaya mno”

Mwandishi: Fürstenau, Marcel
Tafsiri: Bruce Amani
Mhariri: Iddi Ssessanga

LINK: