1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa Jumuiya ya Kiarabu waenda Syria

26 Oktoba 2011

Waandamanaji 13 wameuwawa hivi leo nchini Syria, wakati Rais Bashar Al-Assad wa nchi hiyo akikutana na ujumbe wa mawaziri kutoka Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wanaomshinikiza kuzungumza na upinzani.

https://p.dw.com/p/12zkD
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Nabil el-Araby.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Nabil el-Araby.Picha: picture alliance/dpa

Televisheni ya serikali imesema tu kuwa Rais Assad anakutana na mawaziri hao, lakini haikusema undani wa mazungumzo baina yao.

Hata hivyo, televisheni hiyo ikaonesha maelfu ya watu katika uwanja wa Umayyah, wakiandamana kumuunga mkono Rais Assad. Wakiwa wamebeba bendera za nchi yao, watu hao waliimba nyimbo za kumsifu Rais Assad.

"Tunachotarajia ni kuwa vurugu zitamalizika, mazungumzo yataanza na mabadiko yatafanyika." Amesema Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Nabil El-Araby.

Ujumbe huo unaoongozwa na Qatar, unawajumuisha pia mawaziri wa mambo ya nje kutoka Misri, Algeria, Oman, Sudan na Yemen. Tayari serikali ya Assad imeshasema kwamba iko tayari kwa mabadiliko, lakini inawalaumu wapiganaji wenye silaha kwa kuzihujumu hatua zake za kuleta mageuzi kwa njia za amani.

Raia na wanajeshi wauawa

Vikosi vya serikali ya Syria katika mji wa Homs.
Vikosi vya serikali ya Syria katika mji wa Homs.Picha: picture-alliance/dpa

Hata hivyo, upinzani unasema kwamba kamwe Rais Assad hana dhamira ya kuachia madaraka, wakitaja kuongezeka kwa mauaji, mateso na kukamatwa ovyo kwa raia.

Katika mji wa Homs, kulifanyika mgomo kupinga ukandamizaji wa kijeshi dhidi ya waandamanaji katika kipindi hiki cha miezi saba ya maandamano. Katika mji huo wa wakaazi milioni moja, maduka mengi yalifungwa na wafanyakazi wa sekta za umma na binafsi kubakia majumbani mwao.

Mkaazi mmoja ameliambia Shirika la Habari la Reuters kwamba kuwepo kwa majibizano ya risasi kati ya wapinzani wenye silaha na majeshi ya Assad, kuliongezea mafanikio ya mgomo huu.

Kwa uchache watu wanne wameuawa katika majibizano hayo. Mgomo pia umefanyika katika mji wa Deraa, ambako wakaazi wanasema kwamba ulifanikiwa vyema.

Katika mji wa Hamrat, ulio kaskazini mwa Homs, wanajeshi walioasi wamewauwa wanajeshi tisa wa serikali, baada ya kulishambulia basi lililobeba wanajeshi hao kwa roketi. Haya ni mashambulizi ya karibuni zaidi tangu uasi wa kijeshi uanze.

Assad azidi kubanwa

Waandamanaji wa Syria wakimfananisha Assad na Muammar Gaddafi.
Waandamanaji wa Syria wakimfananisha Assad na Muammar Gaddafi.Picha: dapd

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limesema kwamba ujumbe wa Jumuiya ya Kiarabu kwa Rais Assad unapaswa kuitaka Syria kuruhusu wachunguzi huru wa matukio ya uvunjwaji wa haki za binaadamu nchini humo.

Mkurugenzi wa shirika hilo kwa Mashariki ya Kati, Sarah Leah, amesema njia pekee ya kuhakikisha kuwa raia wanalindwa ni kuwa na waangalizi ndani ya Syria "ambao kuwepo kwao kunaweza kuzuia ukandamizaji wa vikosi vya serikali dhidi ya raia hao."

Kwa upande mwengine, Rais Assad anaendelea kukabiliwa na shinikizo kutoka jumuiya ya kimataifa, ambapo Marekani na Umoja wa Ulaya wameongeza vikwazo vyao dhidi ya mafuta na biashara nyengine za nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Allain Juppe, amesema kwamba mbinyo huu "hatimaye utafanikiwa kuuangusha utawala aliouita wa kikandamizaji."

Hata hivyo, Juppe amekiri kwamba itachukuwa muda mrefu, huku kukiwa na dalili za Syria kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe na mataifa jirani yakikataa uingiliaji kati wa kijeshi kutoka nje.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/AP
Mhariri: Othman Miraji