1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukame waleta athari jimboni Marsabit nchini Kenya

Michael Kwena18 Januari 2022

Serikali ya jimbo la Marsabit imeanza kusambaza chakula cha msaada kwa waathiriwa wa baa la njaa katika jimbo hilo, huku mtu mmoja akiripotiwa kufariki kutokana na makali ya njaa yananayoshuhudiwa kwa sasa jimboni humo.

https://p.dw.com/p/45hbU
Kenia die Dürre hat eine verheerende Wirkung auf den Haustierbestand
Picha: Ed Ram/Getty Images

Haya yanajiri miezi mitatu baada ya serikali ya kenya kuzindua mpango wa shilingi bilioni mbili kusaidia majimbo yaliyoathirika na ukame nchini humo.

Wakaazi katika jimbo la Marsabit wamekuwa wakihangaika kwa miezi kadhaa sasa kufuatia hali ya ukame inayoendelea kushuhudiwa hapa. Hali hii kulingana na wakaazi wa eneo la Gas katika eneo bunge la Horr Kaskazini, tayari imesababisha kifo cha mmoja wao.

Kwa mujibu wa mwakilishi wadi wa eneo hilo Tura Elema,mzee mwenye umri wa miaka sitini na tisa alifariki kwa kukosa chakula eneo la Gas.

"Tumekuwa na changamoto sana na hata mtu alifariki. Alikuwa mzee na alifariki eneo la Gas kutokana na njaa.Tunapata ripoti nyingi kutoka huko na kuna baadhi yao wanaozirai na ndiyo maana tunahitaji msaada wa haraka”

Serikali imebaini hali ya kiangazi katika jimbo hili kama inayochochea mizozo kati ya binadamu na wanyapori.

Naibu kamishna wa marsabit ya Kati David Saruni,ameeleza kwamba,serikali kwa ushirikiano na mamlaka ya kukabiliana na majanga nchini NDMA imekuwa ikitoa msaada wa chakula kwa wahanga wa baa la njaa Pamoja na kuwapa fedha za kujikimu.

Screenshot Kenia Marsabit Trockenheit
Mkaazi wa Marsabit KenyaPicha: Mariel Müller/DW

"Hii njaa bado inaendelea japo tulipata mvua chache hapa marsabit,bado hakuna mavuno kwa hivyo tutaendelea kufanya juu chini ili chakula kipatikane”

Na kama sehemu ya juhudi za kuwanusuru wakaazi wake dhidi ya makali ya njaa,serikali ya kaunti imeanza kuwapa chakula watu walioathirika.

Mohammed Ali ni gavana wa jimbo hili la Marsabit

"Kaunti yetu ni mojawapo ya maeneo kame na mifugo yetu imeanza kufa na watu wana njaa kila sehemu kwa hivyo,inabidi tuangalie kama serikali”

Kiongozi huyo wa kaunti aidha amemtaka rais Uhuru Kenyatta kuchunguza jinsi shilingi bilioni mbili zilizotengewa kaunti zilizoathirika na ukame zilivyotumika.

Jimbo la Marsabit limekumbwa na changamoto kubwa ikiwemo uvamizi wa nzige mwaka jana sawia na ukosefu wa mvua ambayo imepelekea mamia ya mifugo kuangamia.