1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukanda huru wa biashara Afrika wazinduliwa

Lilian Mtono
8 Julai 2019

Viongozi wa Afrika wamezindua mpango wa bara hilo kuwa kanda ya biashara huru, ambao iwapo utatekelezwa kwa mafanikio utawaunganisha watu bilioni 1.3 barani humo.

https://p.dw.com/p/3Lk1W
African Union summit
Picha: Getty Images/I. Sanogo

Mkataba huo pia unatarajiwa kutengeneza kundi la kanda ya kiuchumi yenye thamani ya kiasi cha dola trilioni 3.4, na kuwa mwanzo mpya wa enzi ya maendeleo kwenye bara hilo.

Baada ya miaka minne ya mazungumzo, hatimaye makubaliano ya kuanzishwa kwa ukanda huru wa kibiashara unaojumuisha mataifa 55 ya Afrika yalifikiwa mnamo mwezi Machi, hatua ya kufungua njia ya kuanzishwa kwa ukanda huo kwenye mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika ilifanyika nchini Niger, ambako Ghana ilitangazwa kuwa mwenyeji  wa makao makuu wa Umoja huo na majadiliano yalifanyika juu ya vipi makubaliano hayo yatafanya kazi.

Inatarajiwa chini ya mkataba huo ujulikanao kama AfCFTA, na ambao ni mkubwa kabisa tangu kulipoanzishwa mkataba wa biashara huru wa kimataifa mwaka 1994, utasaidia kuibua na kuimarisha mashirikiano ya kibiashara, mnyororo wa usambazaji bidhaa na utaalamu miongoni mwa bara hilo.

Symbolbild Ägypten Präsident Abdel-Fattah el-Sissi
Rais wa Misri na mwenyekiti wa AU, Abdel Fattah al-Sissi amesifu hatua hiyo aliyoitaja ni mwanzo mzuri.Picha: picture-alliance/AP Photo/MENA

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi, ambaye pia ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, na mwenyekiti wa tume ya umoja huo Moussa Faki Mahamat walikuwa miongoni mwa waliozinduwa rasmi mkataba huo. Na baadae, rais al-Sissi akasema, "Tuko katika njia nzuri kuelekea hali bora ya baadaye. Kuazishwa kwa ukanda huu wa biashara huru kunafungua dirisha jipya la maendeleo na  ufanisi  badala ya mkwamo wa kiuchumi pamoja na mizozo."

Aliongeza kuwa macho ya ulimwengu sasa yanageukia Afrika.

Flash-Galerie HIV / Aids 2010
Wachumi wanaonya kuhusu urasimu wa mipakani unaoweza kuzuia utekelezwaji wa mkatabaPicha: AP

Kulingana na wanauchumi, Afrika bado inakabiliwa na changamoto kubwa, ambazo ni pamoja na ubovu wa barabara zinazounganisha mataifa ya bara hilo, mizozo katika maeneo mengi, urasimu uliopitiliza wa mipakani na rushwa ndogondogo, ambavyo kwa pamoja vinarudisha nyuma ukuaji na utangamano.

Wajumbe kwenye mkutano huo wa 12 usio wa kawaida wa kilele wamekubaliana kuondoa ushuru kwenye bidhaa nyingi, ili kuongeza biashara baina ya mataifa kwa kati ya asilimia 12 hadi 25, katika kipindi cha kati lakini kulingana makadirio ya shirika la fedha duniani, IMF hiyo ingeongeza kwa zaidi ya mara mbili, iwapo changamoto hizo zingekabiliwa vilivyo.

IMF, kwenye ripoti yake ya mwezi Mei imeelezea umuhimu wa ukanda wa biashara huru katika kwenye mabadiliko ya kiuchumi, na kusema kwa kiasi kikubwa umechangia kuimarika kwa ukuaji barani Ulaya na Amerika Kaskazini, lakini ikionya kuondoshwa kwa ushuru pekee haitoshi.

Eritrea ambayo pekee haijasaini makubaliano hayo, imesema itazingatia kusaini makubaliano hayo. AU inakadiria kwamba makubaliano hayo yanayoondoa ushuru baina ya mataifa hayo, yatachangia kuimarika kwa biashara ya ndani kwa asilimia 60 ifikapo mwaka 2022.