1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukimya mjini Cairo, idadi ya vifo yaongezeka

Admin.WagnerD15 Agosti 2013

Mji mkuu wa Misri Cairo unaripotiwa kuwa na utulivu asubuhi ya leo, baada ya operesheni ya kijeshi hapo jana, ambayo iliuwa watu zaidi ya 525. Udugu wa kiislamu umepanga maandamano zaidi mchana wa leo.

https://p.dw.com/p/19QN7
Ulinzi umeimarishwa mjini Cairo baada ya ghasia za jana
Ulinzi umeimarishwa mjini Cairo baada ya ghasia za janaPicha: KHALED DESOUKI/AFP/Getty Images

Asubuhi ya leo mitaa ya Cairo ambayo kwa kawaida huwa na msongamano mkubwa wa magari ilikuwa mitupu, baada ya tangazo la hali ya hatari lililoanza kutekelezwa usiku wa kuamkia leo. Vyombo vya habari nchini Misri vimesema kuwa benki, soko la hisa na posta vitafunga milango leo, kwa hofu kuwa ghasia zaidi zaweza kutokea.

Ulinzi wa kijeshi umeimarishwa kando kando ya barabara muhimu na ofisi za serikali, na jeshi limesema halitakuwa na mzaha katika kuhakikisha kuwa sheria ya hali ya hatari inaheshimiwa, hilo likiwa onyo la wazi kwa wafuasi wa kundi la udugu wa kiislamu ambao wanaweza kujaribu kuonyesha ukaidi.

Idadi ya vifo yazidi kuongezeka

Tangazo la hivi karibuni kutoka maafisa wa wizara ya afya limesema kuwa watu 525 waliuawa katika operesheni ya jana, iliyoendeshwa na jeshi kuwafurusha waandamanaji wanaotaka Mohamed Mursi arejeshwe madarakani. Tangazo hilo lilisema kuwa watu 137 waliuawa katika kambi ya Rabaa al-Adawiya, 57 walipoteza maisha katika uwanja wa al-Nahda, na 227 waliuawa katika maeneo mengine ya nchi. Udugu wa kiislamu umesema takribani watu 2,600 waliuawa jana.

Idadi ya waliokufa inazidi kuongezeka
Idadi ya waliokufa inazidi kuongezekaPicha: Reuters

Umwagaji damu huo umelaaniwa kutoka pande mbali mbali za dunia. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry alisema mauaji hayo hayakubaliki, na yanapaswa kulaaniwa vikali. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle aliitaka serikali ya Misri siyo tu kutoa uhuru wa maandamano ya amani, bali pia kuhakikisha usalama wa waandamanaji. Rais wa Ufaransa Francois Hollande amemuita balozi wa Misri nchini humo, kumtaka atoe maelezo kuhusu umwagaji damu huo wa jana.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ametaka usalama wa waandamanaji uhakikishwe
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ametaka usalama wa waandamanaji uhakikishwePicha: Reuters

Denmark imetangaza kuwa imesimamisha msaada wake wa Maendeleo kwa Misri, kudhihirisha kukerwa kwake na umwagaji damu uliotokana na operesheni ya jana mjini Cairo.

Wakristo walengwa kwa kisasi

Huku hayo yakiarifiwa, makanisa kadhaa ya madhehebu ya kikoptiki yamechomwa moto na wafuasi wa udugu wa kiislamu, kama kisasi kwa mkuu wa madhehebu hayo Papa Tawodros, ambaye aliunga mkono mapinduzi ya kijeshi yaliyomuangusha rais Mohamed Mursi. Shirika la habari la Misri MENA, limesema kuwa wakristo katika miji ya Minya,

Sohag na Assiut walilazimika kukimbia kupitia mapaa ya kanisa, baada ya kuvamiwa na umati wa watu wenye hasira.

Taarifa zaidi zimeeleza kuwa serikali ya Misri imekifunga kivuko kati ya nchi hiyo na ukanda wa Gaza, kwa kile ilichokieleza kuwa sababu za kiusalama.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APDPA

Mhariri: Josephat Charo