1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yatoa wito wa usaidizi kwa kansela wa Ujerumani

Amina Mjahid
15 Januari 2020

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ameiomba Ujerumani kupitia kansela wake Angela Merkel. kuiunga mkono kuhakikisha wale waliohusika katika udunguaji wa ndege ya Ukraine nchini Iran wanawajibishwa.

https://p.dw.com/p/3WFQn
Wolodymyr Selenskyj ukrainischer Präsident
Picha: Getty Images/AFP/G. Ivuskans

Baada ya kukataa kuhusika, Iran hatimae ilikiri siku ya Jumamosi kuwa iliilenga kwa bahati mbaya, ndege ya abiria ya Ukraine na kusababisha vifo vya abiria wote 176. Ndege hiyo ililengwa muda mfupi baada ya kupaa angani

Katika maongezi yake ya simu na Kansela Angela Merkel, Zelenskiy amesema anatarajia waliohusika watashitakiwa na familia pamoja na shirika la ndege kulipwa fidia.  Rais wa Ukraine ameitolea wito Ujerumani kuchangia kisiasa katika mchakato huu.

Ukraine inajaribu kuona iwapo Iran itakubali kuipa kijisanduku cheusi kinachoelezea kile kilichotokea ndani ya ndege kabla ya kupata ajali.

Huku hayo yakiarifiwa rais wa Iran Hassan Rouhani ametoa wito wa umoja na kuelezea umuhimu wa kuwa na mabadiliko ya namna Iran inavyoendesha shughuli zake baada ya waandamanaji waliojawa na hasira kumiminika barabara kufuatia tukio la kuangushwa kwa ndege ya Ukraine.

Rouhani amesema iwapo kulikuwa na ucheleweshwaji kwa upande wa jeshi juu ya ajali hiyo basi ni vyema wakaomba radhi. Waandamanaji wanataka wale wote waliohusika kujiuzulu au kushitakiwa.

Rais wa Iran Hassan Rouhani atoa Onyo kwa Umoja wa Ulaya

Teheran Hassan Ruhani Präsident Iran
Rais wa Iran Hassan Rouhani Picha: picture alliance/dpa/Iranian Presidency

Kando na hilo rais Rouhani ameuhimiza Umoja wa Ulaya kujizuwiya kuchukua hatua isiyofaa katika suala la makubaliano ya Nyuklia yaliotiwa saini mwaka 2015, baada ya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kuongeza shinikizo kwa Jamhuri hiyo ya kiislamu  kwa kuanzisha mfumo wa kutatua migogoro. Rouhani ameuambia Umoja wa Ulaya iwapo utachukua hatua isiyosahihi basi utakuwa hatarini.

Umoja wa Ulaya ilizindua mfumo wa kutatua migogoro hapo jana ili kuishinikiza Iran kuacha kukiuka makubaliano ya nyuklia. Lakini makubaliano hayo yaliotiwa saini kati ya Iran na mataifa sita yalio na nguvu duniani, yamekuwa yakiyumba kuanzia mwaka 2018 baada ya Marekani kutangaza kujiondoa na kuiwekea Iran vikwazo zaidi vya kiuchumi.

January 5 Iran ilisema haioni haja ya kuendelea kuwepo katika makubaliano hayo baada ya Marekani kumuua kamanda wake mkuu Jenerali  Qassem Soleimani katika shambulizi la angani.

Kwengineko mwanamfalme wa Jordan Abdullah wa pili ameonya hii leo kwamba vita kati ya Marekani na Iran vitaleta uharibifu mkubwa duniani.

Katika hotuba yake kwa wabunge wa Umoja wa Ulaya juu ya mvutano unanozidi kupamba moto Mashariki ya Kati, mfalme Abdulla amesema licha ya kwamba Marekani na Iran zimepunguza makali ya vita vyao baada ya baada ya visa vya kulipiziana kisasi ndani ya wiki mbili zilizopita hatari ya mgogoro Mashariki ya Kati iko pale pale.

Chanzo: afp/ap/Reuters/dpa