1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yatakiwa kuunda serikali ya umoja wa Kitaifa

23 Februari 2014

Ikulu ya Marekani imeitaka Ukraine kuchukua hatua za haraka kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na kusaidia kurejesha utulivu baada ya wimbi la ghasia zilizosababisha mauaji.

https://p.dw.com/p/1BDzZ
Ukraine Julia Timoschenko Rede Maidan 22. Feb. 2014
Shangwe katika uwanja wa Maidan, "Uhuru" mjini Kiev baada ya utawala kuangushwaPicha: Reuters

Kauli hii ya Marekani inakuja katika wakati ambapo mwenendo wa mambo nchini Ukraine umechukua mwelekeo mpya ndani ya masaa 48 kuanzia jana Jumamosi (22.02.2014). Awali siku ya Ijumaa bunge lilipunguza madaraka ya rais na kupiga kura kumwachilia huru waziri mkuu wa zamani, Yulia Tymoshenko, kutoka jela.

Lakini ilipofika Jumamosi, waandamanaji walichukua udhibiti wa mji mkuu, Kiev, na kuikamata ofisi ya Rais Viktor Yanukovych, wakati bunge likipiga kura kumuondoa madarakani na kuitisha uchaguzi mpya. Yanukovich ameiita hatua hiyo kuwa ni mapinduzi na kusisitiza kuwa hataondoka madarakani.

Ukraine Julia Timoschenko Rede Maidan 22. Feb. 2014
Yulia Tymoshenko ahutubia umati wa watu katika uwanja wa MaidanPicha: Reuters

Miezi kadhaa ya maandamano iligeuka kuwa ya matumizi ya nguvu wiki hii, ambapo watu kadha wameuwawa katika mapambano kati ya waandamanaji na polisi.

Chini ya mpango wa upatanishi wa awali wa Umoja wa Ulaya, viongozi wa waandamanaji na Rais Yanukovich walikuwa wamefikia makubaliano siku ya Ijumaa ya kuunda serikali mpya na kufanya uchaguzi wa mapema.

Ukraine Julia Timoschenko Rede Maidan 22. Feb. 2014
Tymoshenko akihutubiaPicha: AFP/Getty Images

Marekani yahimiza utulivu

Akitoa wito wa utulivu, msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jay Carney, amesema Marekani inahimiza kuundwa haraka kwa serikali ya umoja wa kitaifa itakayojumuisha wataalamu.

"Tumekuwa kila wakati tukitoa wito wa kusitishwa kwa ghasia , mabadiliko ya kikatiba , serikali ya muungano , uchaguzi wa mapema, na hatua za leo zinaweza kutusogeza karibu na lengo hilo, " amesema Carney katika taarifa. " Msingi usio yumba unaoongoza matukio hayo ni kwamba watu wa Ukraine wanataka kuongoza hatima yao."

Marekani pia imekaribisha kuachiwa huru kwa Tymoshenko kutoka jela.

Hali katika taifa hilo lililokuwa jimbo la zamani la iliyokuwa umoja wa Kisovieti, ambalo limegawika kati ya wale wanaotaka nchi hiyo ielekee upande wa Umoja wa Ulaya na wanaotaka kubakia katika himaya ya Urusi, bado ni tete na bado haifahamiki iwapo upinzani umeshinda dhidi ya Yanukovich katika siku ambayo ilikuwa na mfululizo wa matukio mbali mbali, kiasi miezi mitatu tangu nchi hiyo kuingia katika mzozo.

Kiew Maidan Nacht Ruhe
Uwanja wa Uhuru mjini Kiev usikuPicha: Reuters

Bunge laamua

Bunge mjini Kiev liliamua kuchukua madaraka yaliyoachwa na Yanukovich baada ya kuondoka mjini humo na kupiga kura kumuondoa madarakani na kupanga tarehe ya uchaguzi mpya kuwa Mei 25 mwaka huu.

Sambamba na hilo, wabunge pia walimuachia huru Tymoshenko, waziri mkuu wa zamani na muungaji mkuu wa mahusiano ya karibu na Umoja wa Ulaya ambaye alibakia kuwa hasimu mkuu wa Yanukovich hata alipohukumiwa kwenda jela mwaka 2011 katika hukumu ya miaka saba kutokana na matumizi mabaya ya madaraka yake.

Ukraine Protest Ansprache Janukowitsch 19.02.2014
Rais Viktor YanukovichPicha: Reuters

Ufaransa imeikaribisha hatua ya kuachiliwa huru kwa Tymoshenko na kutoa wito kwa pande zote katika taifa hilo lililogawika kisiasa kujizuwia na ghasia zaidi.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Laurent Fabius, ambaye yuko katika ziara ya kiserikali nchini China ameitaka Ukraine kuhakikisha kuwa uchaguzi mpya unafanyika haraka iwezekanavyo.

Mwandishi: Sekione Kitojo/ape/afpe/rtre

Mhariri: Mohammed Khelef