1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukuaji wa kiuchumi unapungua kasi Angola

P.Martin20 Juni 2008

Ukuaji wa kiuchumi unaokwenda pole pole nchini Angola utaathiri vibaya mauzo ya nje ya washirika wake wakuu wa biashara hasa Ureno na Brazil.

https://p.dw.com/p/ENKH

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo-(OECD) inatathmini kuwa kiwango cha ukuaji wa kiuchumi nchini Angola utapunguka kwa asilimia 15 ifikapo mwaka 2009.

Kulinganishwa na miaka ya hapo awali hicho ni kiwango kidogo.Lakini hata hivyo ni pigo kwa Ureno,iliyokuwa mkoloni wa zamani wa Angola-nchi ambayo hivi sasa ina utajiri wa mafuta lakini inapungukiwa fedha taslimu.

Profesa wa uchumi Jorge Braga de Macedo aliewahi kuwa waziri wa fedha nchini Ureno kati ya mwaka 1991 hadi 1993 anasema,mafuta huchangia asilimia 60 ya pato la ndani la Angola na ni asilimia 95 ya mauzo yake ya nje. Kwa hivyo ukuaji wa kiuchumi wa asilimia 5.1 uliotabiriwa kwa mwaka 2009 utaweza kuleta mabadiliko makubwa katika jamii ikiwa faida itakayopatikana itatumiwa kuwanufaisha masikini na vile vile kuzalisha ajira na kutoa vivutio katika sekta ya uchumi wa ndani.

Profesa huyo anasema,litakuwa kosa kubwa kuendelea na mtindo wa hivi sasa usiowafikiria masikini.Kwani kufuatia uchunguzi wa kiuchumi uliofanywa na wataalamu wa maendeleo,serikali ya Rais Jose Eduardo dos Santos inashauriwa kubadilisha mtindo wa hivi sasa unaowabagua masikini katika ukuaji wa uchumi.

Wakati huo huo,Silvio de Paula alie mwekezaji nchini Angola anasema,tangu makubaliano ya amani kutiwa saini mwaka 2006 kufuatia kifo cha kiongozi wa waasi Jonas Savimbi katika mwaka 2002,nchini humo siku hizi kuna kundi dogo la watu waliojikusanyia utajiri uliopindukia kiasi.Kwa upande mwingine baadhi kubwa ya umma huishi na njaa na katika hali ya umasikini mkubwa katika nchi iliyo na uwezo wa kuwa miongoni mwa mataifa tajiri kabisa duniani.

De Paula anasema,si viongozi wa chama cha kikomunisti cha zamani MPLA tu wanaonufaika kutokana na utajiri wa Angola,bali hata waasi wa zamani wa chama cha UNITA hupokea kitita chao pia.Waandishi wa habari wanaoripoti juu ya hali hiyo hufikishwa mahakamani ikiwa ni mwananchi wa Angola au anapokuwa raia wa Ureno hutishiwa kufukuzwa Angola.

Kampuni kubwa kabisa ya mafuta ya Kimarekani,Chevron itawekeza jumla ya dola bilioni 20 barani Afrika katika miaka mitano ijayo ili kuzidisha uzalishaji wa mafuta na gesi ya ardhini hasa nchini Angola na Nigeria.Barani Afrika,baada ya Nigeria,Angola inachukua nafasi ya pili kama mzalishaji mkubwa kabisa wa mafuta kusini mwa Sahara.