1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

280108 Brüssel EU-Außenminister

Maja Dreyer28 Januari 2008

Kenya na Chad, Gaza na Kosovo - kwenye mkutano wao wa leo mawaziri wa masuala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya walikuwa na mada nyingi muhimu ya kuzungumzia.

https://p.dw.com/p/Cyt4
Picha: AP



Katika azimio lao la pamoja, mawaziri wa masuala ya kigeni wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kwa njia isiyo wazi walitishia kupunguza misaada yake kwa Kenya. Azimio hili linasema na ninanukuu: IKiwa suluhisho la kudumu linalokubaliwa na wote halitapatikana, hilo litaathiri kujitokeza kwa nchi wafadhili katika Kenya pamoja na uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Kenya. Mawaziri hawa walisikitishwa kwamba licha ya juhudi za wapatanishi wa kimataifa, hali badi ni mbaya. Kenia inatarajiwa kupata Euro Millioni 383 katika muda wa miaka mitano ijayo kama msaada wa maendeleo kutoka kwa Umoja wa Ulaya.


Kwenye mkutano wao, mawaziri wa kigeni wa Umoja wa Ulaya waliamua pia kuhusu kutumwa kikosi cha kulinda usalama nchini Tshad ili kuzuia vita vya Darfur visienee hadi Tshad. Mhusika wa masuala ya kigeni, Javier Solana alisema wanajeshi hao ambao hawatapungua 3500 watakuwepo Tshad kabla ya msimu wa mvua kuanza na watapelekwa huko kuanzia wiki zijazo. Muda wa kubakia Tshad umewekwa kwa mwaka mmoja kwa sasa.  Jukumu la kikosi hiki ni kuzuia mashambulizi dhidi ya wakimbizi wa Darfur walioko Tshad.


Suala muhimu la mkutano huu wa leo lilikuwa lile la Serbia na uhusiano wake na Umoja wa Ulaya. Siku sita kabla ya uchaguzi wa rais nchi Serbia, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya bado hazikubaliani kuhusu namna na kuendelea na mazungumzo na serikali ya nchi hii ya Mashariki ya Ulaya. Kinyume na matamshi ya awali, mkataba wa kuimarisha usalama na uhusiano na Umoja wa Ulaya hautatiwa saini. Uholanzi na Belgium zilipinga mkataba huu kwa sababu Serbia haikubali kuiunga mkono mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita na kupeleka kwa mahakama watuhumiwa wahalifu wa kivita Ratko Mladic na Radovan Karadizic. Mkataba huu unaangaliwa kuwa hatua muhimu kuelekea Serbia kuweza kujiunga na Umoja wa Ulaya.


Umoja wa Ulaya leo pia ilitoa mwito kwa Israel kutekeleza jukumu lake mbele ya eneo la ukanda wa Gaza. Serikali za Ulaya ziko na wasiwasi kuhusu hali ya binadamu katika eneo la Gaza, azimio la leo linasema. Pia zimedai kupelekwa kwa bidhaa za kuhakikisha maisha ya watu pamoja na nishati na mafuta. Waziri wa masuala ya kigeni wa Ujerumani, Franz-Walter Steinmeier alisema pia anasikitishwa na namna kundi la Hamas linavyotendea hofu na maafa ya wananchi wake. Wapalestina wa Gaza wanapaswa wenyewe kutuliza hali na kuwasitisha wao wanaoishambulia Israel.  Katika azimio lao, mawaziri hawa wa Ulaya walitambua haki ya Israel kujilinda, lakini walitaka kumaliza hatua zozote za kutumia nguvu. Pande zote za vita zinatakiwa kujitahidi mipaka ifunguliwe kwa njia halali.