1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yaimarisha vizuizi kukabiliana na corona

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
16 Desemba 2020

Nchi za Ulaya zimeimarisha vizuizi kwa ajili ya kupambana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona hasa wakati huu ambapo sikukuu ya Krismasi inakaribia.Hatua hizo zinatofautiana baina ya nchi na nchi.

https://p.dw.com/p/3mo6p
Themenbilder - Lockdown in Sachsen
Picha: Sabine Kinkartz/DW

Hatua mpya ya kufunga shughuli za kawaida imeanza kutumika nchini Ujerumani Jumatano tarehe 16 Desemba siku ambayo pia nchi hiyo ilishuhudia idadi kubwa zaidi ya vifo tangu kuanza kwa janga la virusi vya corona. Jumla ya watu 952 walifariki usiku wa kuamkia siku hiyo kutokana na ugonjwa wa Covid -19.

Ufaransa iliweka amri ya kutotoka nje usiku tangu siku ya Jumanne, amri hiyo inaanza saa mbili usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi, amri hii lakini itaondolewa katika siku ya mkesha wa Krismasi tu na sio siku ya mkesha wa mwaka mpya.

Waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte anatafakari mipango ya kuanzisha tena vizuizi kabla ya Krismasi, lakini amesema nchi yake haitaweka vizuizi vikali kama vya Ujerumani.

Wakati huo huo, matumaini ya kupatikana chanjo ya COVID -19 kabla ya mwisho wa mwaka huu inayotengenezwa na kampuni za Pfizer na BioNtech yameimarika baada ya Umoja wa Ulaya kusogeza karibu hadi tarehe 21 Desemba, ambapo jopo la wataalamu litakutana kuidhinisha utoaji wa chanjo hiyo.

Bango katika mji wa Dortmund la kuhamasisha ununuzi wa mitandaoni kutokana na hatua za karantini kuimarishwa nchini Ujerumani.
Bangokatika mji wa Dortmund la kuhamasisha ununuzi wa mitandaoni kutokana na hatua za karantini kuimarishwa nchini Ujerumani.Picha: Bernd Thissen/dpa/picture alliance

Katika mahojiano na DW mbunge wa chama cha kijani Janosch Dahmen ambaye pia ni daktari amesema Ujerumani ilifanikiwa hapo mwanzoni kudhibiti maambukizi lakini ilifanya ajizi katika msimu wa joto. Amesema Ujerumani haikuchukua hatua za lazima katika msimu huo na hivyo kusababisha ongezeko kubwa la maambukizi hasa miongoni mwa watu waliomo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi. Hata hivyo mbunge huyo ameelezea matumaini ya kuweza kukabiliana na hali hiyo kutokana na kupatikana kwa chanjo. Juu ya kuishughulikia mikakati ya kuirudisha nchi katika hali ya kawaida, Dahmen amesema chanjo tu ndio suluhisho la pekee.

Ustawi wa uchumi

Taasisi maarufu ya utafiti ya mjini Munich (IFO) imeteremsha matarajio yake ya awali ya ustawi wa uchumi wa Ujerumani kwa mwaka 2021 kutoka asilimia 5.1 hadi asilimia 4.2. Taasisi hiyo imebashiri kwamba kustawi tena kwa uchumi kutachelewa hadi mwaka 2022 na inatarajia pato jumla litastawi kutoka asilimia 1.7 hadi asilimia 2.5.

Mkuu wa kitengo cha makadirio kwenye taasisi hiyo ya mjini Munich Timo Wollmershaeuser amesema hatua za kufunga shughuli za kila siku na karantini zilizochukuliwa nchini Ujerumani na kwenye nchi zingine zimerudisha nyuma ustawi wa uchumi. Uzalishaji wa bidhaa na huduma hautafikia kiwango kilichokuwapo kabla ya janga la corona kabla ya mwaka ujao. Amesema pana uwezekano wa mwaka huu kumalizika na upunguaji wa pato jumla la ndani.

Chanzo: https://p.dw.com/p/3mmdV