1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa mambo ya nje wataka hatua kali

Mohammed Khelef19 Januari 2015

Mawaziri wa nje wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels kukiwa na wito ushirikiano wa karibu zaidi kati ya Ulaya na ulimwengu wa Kiarabu katika kukabiliana na makundi ya itikadi kali.

https://p.dw.com/p/1EMkB
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini (kushoto), akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania, Jose Manuel Garcia-Margallo.
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini (kushoto), akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania, Jose Manuel Garcia-Margallo.Picha: Reuters/Y. Herman

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, amesema hivi leo kwamba Ulaya inahitaji kuwa na muungano wa aina fulani na nchi za Kiarabu na kuimarisha njia ambapo pande hizo mbili zinashirikiana.

Mogherini aliyazungumza hayo baada ya kukutana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Nabil el-Arabi, wakati mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wakiwa mjini Brussels kuandaa mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja huo wanaokutana mwezi ujao kuzungumzia tatizo la siasa kali.

Baadhi ya mawaziri hao, akiwemo Philip Hammond wa Uingereza, wamesisitiza umuhimu wa Ulaya kushirikiana na nchi za Kiislamu badala ya kuzilaumu kwa tatizo hilo. Hammond ameongeza kuwa Ulaya kwa ujumla wake imejitolea kufanya kila iwezalo ili iendelee kubaki salama

"Tutaamua kufanya kile kilicho muhimu kuibakisha Ulaya salama dhidi ya vitisho vya magaidi. Jukumu letu ni kuzungumzia changamoto ya makundi ya siasa kali inayotukabili sasa na namna tunavyochukuwa hatua kukabiliana nayo," alisema Hammond.

Hakuna suluhisho bila kukomesha vita Mashariki ya Kati

Hata hivyo, mawaziri wengi wameonesha upinzani mkubwa wa kuundwa kwa sheria mpya dhidi ya siasa kali na ugaidi kufuatia zile zilizotungwa mwaka 2005 baada ya wimbi la mashambulizi kwenye maeneo kadhaa barani Ulaya.

Wanajeshi wakilinda makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels.
Wanajeshi wakilinda makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels.Picha: Reuters/E. Vidal

Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Margot Waalstrom, amesema hakuna suluhisho la haraka dhidi ya changamoto la wapiganaji wa kigeni barani Ulaya, kabla ya kwanza kumaliza vita nchini Syria na Iraq.

Mwenzake wa Ubelgiji, Didier Reynders, ambaye nchi yake ilitegua njama ya mpiganaji mmoja aliyetambuliwa kuwa Muislamu mwenye siasa kali kuwauwa polisi, ametoa wito kwa Bunge la Ulaya kukubaliana na ombi la kuanzisha rikodi ya pamoja ya abiria.

"Ninatazamia kuwa Bunge la Ulaya litabadilisha mtazamo wake na kuamuru kuanzishwa Rikodi ya Majina ya Abiria kwenye kiwango cha Ulaya na pia kwa kushirikiana na wadau wengine kama vile Marekani na Canada," alisema Reynders.

Ikiwa bunge la Ulaya litakubaliana na pendekezo hilo, wasafiri wote wanaovuuka mipaka ya upande mmoja hadi mwengine watakuwa kwenye rikodi ya pamoja kwa mataifa yote wanachama na washirika.

Sehemu ya kwanza ya mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya ilimalizika leo mjini Brussels kwa makubaliano ya kuukatia rufaani uamuzi wa Mahakama ya Umoja wa Ulaya wa hapo Disemba 17, ambao uliliondoa kundi la Hamas kwenye orodha ya makundi ya kigaidi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo