1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu wa soka wamlilia Diego Maradona

26 Novemba 2020

Watu mashuhuri duniani na ulimwengu wa soka kwa ujumla, wanaomboleza kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Argentina Diego Maradona, aliyefariki dunia siku ya Jumatano

https://p.dw.com/p/3lqAu
Diego Maradona | WM Finale 1986
Picha: Carlo Fumagalli/AP Photo/picture alliance

Watu mashuhuri duniani na ulimwengu wa soka kwa ujumla, wanaomboleza kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Argentina Diego Maradona, aliyefariki siku ya Jumatano. Diego Maradona amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 60. Kulingana na msemaji wake, Maradona amefariki dunia kutokana na mshutuko wa moyo, wiki mbili baada ya kuruhusiwa kutoka hopsitali. Mchezaji huyo aliyeiongoza Argentina kutwaa kombe la dunia mwaka 1986, alifanyiwa upasuaji wa ubongo mapema mwezi huu. Maradona aliondoka hospitali baada ya kufanyiwa upasuaji kuondoa damu iliyokuwa imeganda katika ubongo wake, huku wakili wake Matias Moria akisema ulikuwa muujiza kwamba damu hiyo iliyoganda, ambayo ingesababisha kifo chake, ilikuwa imegundulika mapema.Anachukuliwa na mashabiki wa soka kama mmoja wa wachezaji wakubwa kuwahi kutandika kabumbu. Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, Maradona amelazwa hospitali mara tatu kwa hali mbaya ya afya kutokana na utumiaji wa dawa za kulevya na kilevi. Hivi karibuni, alilazimika kukaa karantini nyumbani kutokana na janga la COVID-19. Serikali ya Argentina imetangaza siku tatu za maombolezo.