1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu waichangia Lebanon zaidi ya Euro milioni 250

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
10 Agosti 2020

Viongozi wa ulimwengu wameahidi kuichangia Lebanon zaidi ya Euro milioni 250 baada ya nchi hiyo kukumbwa na milipuko miwili mikubwa kwenye bandari ya mji wa Beirut. Mwenyeji wa mkutano huo Ufaransa imesema,

https://p.dw.com/p/3giTp
Libanon Macron in Beirut
Picha: Reuters/D. Nohra

Viongozi hao wa dunia na mashirika ya kimataifa wametoa ahadi hiyo kwa ajili ya kuisaidiia Lebanon baada ya nchi hiyo kukumbwa na maafa yaliyosababishwa na mlipuko mkubwa. Hata hivyo viongozi na mashirika  hayo yameeleza kwamba fedha hizo zinazokusudiwa kwa ajili ya ujenzi mpya wa mji mkuu wa nchi hiyo Beirut hazitatolewa mpaka viongozi wa Lebanon watakapohakikisha kwamba watafanya mageuzi ya kisiasa na kiuchumi ambayo wananchi wanayataka.

Viongozi walioshiriki kwenye mkutano wa hapo jana walikuwa ni pamoja na rais wa Marekani Donald Trump, Mfalme Abdullah wa pili wa Jordan, rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri, viongozi wa Umoja wa Ulaya na wajumbe kutoka China. Mkutano huo uliongozwa na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa. Washiriki zaidi ya 30 kwenye mkutano huo wa kimataifa waliahidi msaada kwa ajili ya kufanyika uchunguzi wa kuaminika.

Wananchi wa Lebanon waandamana kupinga usimamizi mbaya na ufisadi
Wananchi wa Lebanon waandamana kupinga usimamizi mbaya na ufisadiPicha: Reuters/G. Tomasevic

Watu nchini Lebanon kwenyewe wanataka uchunguzi ufanyike juu ya mlipuko uliotokea wiki iliyopita uliosababisha vifo vya watu wapatao 160. Watu wengine zaidi ya 6000 walijeruhiwa kutokana na mlipuko huo. Wakati huo huo mawaziri kadhaa wamejiuzulu ikiwa ni ishara jinsi serikali ya Lebanon inavyosambaratika. Waziri wa mazingira Demanios Kattar ambaye pia amejizulu amesema serikali ya Lebanon imekwama. Amesema serikali hiyo haina uwezo wa kufanya chochote.

Nchini Lebanon ikiwa idadi ya mawaziri wanaojizulu itafikia saba kati ya 20, baraza la mawaziri litalazimika kujiuzulu na nafasi yake itachukuliwa na serikali ya mpito. Katika kadhia nyingine maandamano yameendeela kwenye mitaa ya mjini Beirut ya watu wanaotaka mageuzi. Mamia ya watu wanawalaumu viongozi wa serikali kwa usimamizi mbovu na kwa ufisadi.

Wakati huo huo Iran imesema maafa ya Lebanon hayapaswi kugeuzwa mtaji wa kisiasa na imeitaka Marekani iondoe vikwazo ilivyoweka dhidi ya Lebanon ikiwa nchi hiyo inayo dhamira ya kweli ya kuisaidia Lebanon.

Vyanzo:/AFP/AP/RTRE