1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UM watishia kuiwekea vikwazo Eritrea.

Halima Nyanza10 Julai 2009

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema litazingatia kuchukua hatua zinazofaa dhidi ya nchi kadhaa, ikiwemo Eritrea, ambazo zinadaiwa kutoa misaada kwa makundi ya wapiganaji nchini Somalia.

https://p.dw.com/p/IkqT
Rais wa Eritrea, Isayas Afewerki, ambaye nchi yake inadaiwa kuwasaidia wapiganaji wa Somalia.Picha: AP

Onyo hilo limetolewa kufuatia wito uliotolewa na Umoja wa Afrika, AU, katika kikao chake cha Ijumaa wiki iliyopita mjini Sirte, Libya, ambapo uliliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuiwekea vikwazo Eritrea kutokana na kuwasaidia wapiganaji wa kiislamu wanaopigana na majeshi ya serikali.


Wito huo ulisisitizwa pia na Shirika la Maendeleo la nchi za Pembe na Mashariki ya Afrika -IGAD.


Serikali ya Somalia na mataifa mengine zimeilaumu Eritrea kwa kuwapatia silaha wapiganaji, jambo ambalo linakwenda kinyume na vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa ambavyo vinaruhusu kusafirisha bidhaa hizo kwa serikali tu.


Hata hivyo, maafisa wa Eritrea wamekanusha madai hayo ya kuwasaidia wapiganaji wa Somalia kwa kusema kuwa hawajawahi kuwapa silaha wapiganaji hao na hata kuisaidia kwa silaha serikali ya Somalia.


Eritrea imeitupia lawama Ethiopia kwa kusambaza uzushi huo, kwa lengo la kutaka kuiweka Eritrea katika hali ngumu, kwa kuwekewa vikwazo.


Nao mabalozi wa Ufaransa na Marekani katika Umoja wa Mataifa waliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba Eritrea imekuwa ikitoa misaada kwa wapiganaji hao, ambapo balozi wa Marekani, Susan Rice, amesema serikali ya Eritrea imekuwa ikiwasaidia wapiganaji hao kifedha, kijeshi na msaada wa kisiasa kwa kundi la Al Shabaab na vikundi vingine vyenye msimamo mkali.


Kwa upande wake, balozi wa Ufaransa, Jean-Maurice Ripert, amesema wapiganaji hao wamekuwa wakiripoti kwamba wamekuwa wakipata silaha kutoka Asmara, na kuongeza kwamba nchi yake imekubali kuweka vikwazo kwa wale wote wanaozuia kuwepo amani.


Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshutumu pia shambulio la hivi karibuni dhidi ya raia na serikali ya mpito nchini humo, ambalo lililofanywa na makundi ya wapiganaji wa kigeni ambao wanadhoofisha amani na uthabiti wa Somalia, shambulio ambalo lilisababisha vifo vya zaidi ya watu 70.


Makundi ya wanamgambo wa Al Shebaab na Hezb al Islam, ambao yamejikita katika siasa za itikadi kali, yalifanya mashambulio makali yasio wahi kutokea nchi nzima dhidi ya utawala wa Rais wa Somalia, Sharif Sheikh Ahmed, ambaye anaungwa mkono na jumuia ya kimataifa.


Baraza hilo limeelezea kubakia na msimamo wa mpango wa amani wa Djibouti iliofikiwa mwaka uliopita kati ya serikali ya mpito na kundi kubwa la upinzani, mpango ambao lakini umeshindwa kuimarisha amani.


Limeelezea wasiwasi wake mkubwa na hali hiyo na kusema kwamba litazingatia kwa haraka, hatua gani ya kuchukua dhidi ya upande wowote unaodhoofisha mpango wa amani wa Djibout.




Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters/AFP)

Mhariri: Othman, Miraji