1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika hautaki Umoja wa mataifa uingilie kati Guinee

Oumilkher Hamidou20 Oktoba 2009

Utawala wa kijeshi wa Guinee unazidi kushinikizwa na walimwengu

https://p.dw.com/p/KB4C
Kiongozi wa kijeshi Dadis Camara na waziri mkuu wa Guinee Kabine KomaraPicha: DPA

Umoja wa Afrika,unaoongozwa hivi sasa na Libya, umepinga "kujiingiza Umoja wa mataifa katika mambo ya ndani ya Guinea,baada ya uamuzi wa kuundwa kamisheni maalum ya kimataifa kuchunguza mauwaji ya September 28 iliyopita.

"Umoja wa Afrika unapinga moja kwa moja mtindo huo,unaouangalia kua ni sawa na kuingilia mambo ya ndani ya nchi huru" amesema hayo msemaji wa ofisi ya mwenyekiti wa Umoja wa Afrika,aliyenukuliwa na shirika la habari la Libya-JANA.

Mbinu zozote za kuingilia kati Umoja wa mataifa zitaangaliwa kama "upotovu mbaya sana wa tume za jumuia hii ya kimataifa"msemaji huyo ameongeza kusema.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika amezitolea mwito pande zote ziheshimu uhuru wa Guinea na kuacha kuingilia kati katika mambo ya ndani ya nchi hiyo.Amemaliza kusema.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon ameamua ijumaa iliyopita kuunda kamisheni ya kimataifa kuchunguza matumizi ya nguvu yaliyofanywa na wanajeshi dhidi ya upande wa upinzani mjini Conakry September 28 iliyopita.Kwa mujibu wa Umoja wa mataifa watu zaidi ya 157 waliuwawa.

Mjumbe maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa aliyepewa jukumu la kutayarisha njia ya kuanzishwa uchunguzi huo,Haile Menkerios alifanya ziara ya siku mbili mjini Conakry ambapo alizungumza kwanza na waziri mkuu wa Guinee Kabiné Komara,viongozi wa upande wa upinzani na baadae alikutana na kiongozi wa utawala wa kijeshi Moussa Dadis Camara.Kabla ya kuondoka hapo jana naibu katibu mkuu huyo wa Umoja wa mataifa alizungumza na mabalozi wa nchi tofauti mjini Conakry.

Kufuatia shinikizo la kimataifa kiongozi wa kijeshi wa Guinea Dadis Camara ameamua pia uchunguzi ufanyike katika daraja ya kitaifa.

Umoja wa Afrika ambao sawa na jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi ya Afrika magharibi-ECOWAS, inatishia kuwawekea vikwazo watawala wa kijeshi,wanamtaka kepteni Dadis Camara asipiganie kiti cha rais uchaguzi utakapoitishwa mwakani.

Vikwazo hivyo ni pamoja na kuzuwiliwa wasisafiri viongozi wa utawala wa kijeshi CNDD na kuzuwiliwa mali zao.Kuhusu vitisho hivyo na kama Guinea inaelemea zaidi upande wa kamisheni moja ya uchunguzi au nyengine,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Guinee anasema:

"Hasha hatuna chuki yoyote kati ya kamisheni zilizopo.Kila moja ina shabaha moja nayo ni kuwasaka wahusika na kuhakikisha kisa kama kile hakitokei tena nchini Guinea."

Baada ya mazungumzo yake mjini Conakry,mjumbe maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa,Haile Menkerios alituwa kwa muda mjini Ouagadougou kwa mazungumzo pamoja na mpatanishi wa mzozo wa Guinea,rais Blaise Compaore wa Burkina Fasso.

Mwandishi: Oummilkheir Hamidou/AFP

Mhariri:M.Abdul-Rahman