1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika waisimamisha uanachama Guinea kwa muda

Saleh Mwanamilongo
10 Septemba 2021

Umoja wa Afrika umeisimamisha uanachama Guinea kufuatia mapinduzi ya kijeshi. Wakati huo huo, Jumuiya ya Ecowas,imepeleka ujumbe wa kidiplomasia nchini humo.

https://p.dw.com/p/40Akq
Flagge der Afrikanischen Union
Picha: Klaus Steinkamp/McPHOTO/imago images

Kupitia mtandao wake wa Twitter Umoja wa Afrika umesema umeisimamisha Guinea kutoka shughuli zote na mabaraza yote ya kupitisha maamuzi ya umoja huo. Hatua ya Umoja wa Afrika imekuja siku tano baada ya vikosi maalum vya Guinea kutwaa madaraka kwa nguvu na kumkamata rais Alpha Condé.

Mnamo siku ya Jumapili, Umoja wa Afrika ulilaani hatua hiyo ya jeshi na kutoa wito wa kuachiliwa kwa Condé, ambaye ni rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini humo mwaka 2010.

Baraza la masuala ya Kisiasa, Amani na Usalama ya AU imemtaka Mkuu wa Kamisheni ya umoja huo Moussa Faki kushirikiana na wadau katika kanda hilo juu ya mgogoro huo wa Guinea. Uamuzi huo wa Umoja wa Afrika umetolewa siku moja baada ya marais wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi ECOWAS kuchukua hatua kama hiyo. Lakini Waguinea wamezipokea hatua hizo kwa shingo upande.

''Ecowas ilifanya nini kwa Waguinea?''

Mapinduzi ya Jumapili yamekosolewa na Marekani, Umoja wa Ulaya na jumuiya ya ECOWAS.
Mapinduzi ya Jumapili yamekosolewa na Marekani, Umoja wa Ulaya na jumuiya ya ECOWAS.Picha: Pius Utomi Ekpei/AFP/Getty Images

Faya Koundouno, mbunge wa zamani wa Conakry amesema raia wa Guinea wamechoshwa na unafiki wa Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Ecowas.

"ECOWAS haina funzo la kutupatia. Tunaamini kwamba watu wa Guinea wamebeba dhamana kwa ajili ya historia ya nchi yao. ECOWAS haiijali Guinea. Wakati Condé alikuwa akivuruga katiba kwa ajili ya muhula wa tatu, ECOWAS ilifanya nini? Haikufanya chocote. Kwa hivyo hawapaswi kujitokeza hivi sasa.",alisema Koundouno.

Waziri MKuu  mpya wa kiraia

Ujumbe kutoka Ecowas uliwasili leo Ijumaa mjini Conakry, mji mkuu wa Guinea kwa ajili ya mazungumzo na viongozi wapya wa kijeshi. Lengo la mazungumzo hayo ni kuwashawishi wanajeshi kurejesha utawala wa kiraia nchini humo. Afisa mwandamizi wa jumuiya ya Ecowas amesema uongozi wa kijeshi ni lazima imteue haraka iwezekanavyo Waziri Mkuu mpya ambaye sio mwanajeshi.

Ujumbe wa jumuiya ya Ecowas unaongozwa na Rais wa halmashauri ya jumuiya hiyo, Jean-Claude Kassi Brou, waziri wa mambo ya nje wa Ghana Shirley Ayorkor Botchway na waziri wa mambo ya nje wa Burkina Faso, Alpha Barry.

Mnamo kipindi cha mwaka mmoja, Ecowas imeshuhudia mapinduzi matatu ya kijeshi, ikiwemo mara mbili nchini Mali.