1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa kuzindua ripoti ya viumbe hai

Grace Kabogo
6 Mei 2019

Umoja wa Mataifa leo unazindua ripoti yake ya kisayansi kuhusu viumbe hai, ambayo itaangazia kitisho cha kuangamia kwa aina ya mimea duniani pamoja na wanyama na maana yake kwa binadamu.

https://p.dw.com/p/3Hz8V
Symbolbild Artensterben Korallen
Picha: Getty Images/D. Miralle

Mwenyekiti wa ripoti hiyo yenye zaidi ya kurasa 1,000, Robert Watson amesema kuwa kuna vitisho vikubwa vitano dhidi ya viumbe hai, ikiwemo uharibifu wa misitu na majani katika mashamba; uvuvi uliokithiri katika bahari; mabadiliko ya tabia nchi pamoja na uchafuzi wa mazingira na kuenea kwa viumbe vamizi.

Watson amesema serikali zinaanza kulichukulia suala hilo kwa umakini mkubwa kwa sababu kama wasipoweza kutafuta ufumbuzi wa kitisho hicho kwa sasa, dunia inaweza ikaishia kuwa inayokabiliwa na njaa pamoja na kiu.

''Viumbe vya asili ni mali kubwa sana ambavyo tunavyo na vinavyohitaji kusimamiwa vizuri na usimamizi huo ukiwa endelevu, utausaidia uchumi wetu kukua, utatusaidia na ajira. Lakini swali ni je: kwa kiwango gani shughuli za binaadamu zinaweza kufanikisha katika kusimamia viumbe vya asili,'' aliuliza Watson.

Spanien Waldbrand in der Nähe des Donana National Park
Msitu ukichomwa moto kusini mwa UhispaniaPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Diaz

Kwa wiki nzima iliyopita wanasayansi kutoka mataifa 130 walikutana mjini Paris, Ufaransa ili kukubaliana kuhusu taarifa ya mamlaka. Muhtasari wa mkutano huo kuhusu Jukwaa la sera ya Kisayansi juu ya huduma na mfumo wa viumbe hai, unapaswa kuidhinishwa kwa sauti moja na zaidi ya nchi 100.

Wakati mkutano huo ulipoanza, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Audrey Azoulay aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba ripoti hiyo itawalazimisha kukabiliana na uharibifu mkubwa wa viumbe hai na kushirikishana ushahidi huo na jamii kwa ujumla.

Wanasayansi wanasema viumbe vya asili viko katika hatari zaidi sasa kuliko muda wowote ule katika historia ya binadamu, ambapo zaidi ya viumbe milioni moja vya mimea na wanyama vimepungua. Watafiti wanasema kwamba tatizo hilo linakumbushia ubinaadamu, lakini bado dunia haijachelewa kulitafutia ufumbuzi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya mataifa yameathirika vibaya na kitisho hicho vikiwemo visiwa vidogo. Rebecca Shaw, mwanasayansi mkuu wa Shirika la Wanyamapori WWF anasema nchi nyingine kama vile Marekani zilikuwa makini katika kile inachokifanya, lakjini zilikubaliana kwamba ''ziko hatarini''.

Shaw ambaye alishuhudia majadiliano ya mwisho anasema wito huu una umuhimu mkubwa sana kwa kubadilisha mwenendo wa maisha ya mwanadamu, ili kuzuia kupotea kwa viumbe vya asili.