1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wailaumu Ulaya kwa vifo vya wahamiaji

Mohammed Khelef
26 Mei 2021

Umoja wa Mataifa umeukosoa Umoja wa Ulaya kwa uvunjaji wa haki za binaadamu kupitia sera zake za uhamiaji ambazo hupelekea maelfu ya wahamiaji kukumbwa na maafa wakiwania kuingia Ulaya kusaka hifadhi.

https://p.dw.com/p/3tyCB
Michelle Bachelet | UN Hochkommissarin für Menschenrechte
Picha: picture-alliance/Keystone/S. Di Nolfi

Ripoti iliyowasilishwa siku ya Jumatano (Mei 26) Geneva kwenye makao makuu ya Ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, ilitupa lawama kwa Umoja wa Ulaya na taasisi zake kwa kushindwa kuwalinda watu kwenye matukio kadhaa ya uhamiaji, ikisema ni matokeo ya "maamuzi na sera za Ulaya, mataifa wanachama na pia mamlaka nchini Libya", ambako wahamiaji hao huondokea.

Ripoti hiyo ya kurasa 37 iliyopewa jina la "Upuuziaji: Msako na uokozi na ulinzi wa wahamiaji kwenye Bahari ya Kati ya Mediterenia" ilizungumzia kipindi cha baina ya Januari 2019 hadi Disemba 2020. 

"Msiba hasa ni kwamba mateso na vifo vingi vinavyotokea kwenye njia ya kati ya Bahari ya Mediterenia vinaepukika," alisema Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet, wakati wa kuwasilishwa kwa ripoti hiyo.

Kamishna huyo aliutaka Umoja wa Ulaya kuimarisha huduma zake za uokozi kati ya Libya na mataifa wanachama, akisema usipofanya hivyo, basi Ulaya itakuwa inawapora kwa makusudi wahamiaji hao haki za kimsingi za kibinaadamu, heshima na, katika baadhi ya wakati, hata roho zao.

Kwa mwaka 2020 pekee, wahamiaji 632 wamepoteza maisha kwenye Bahari ya Mediterenia wakiwania kuingia Ulaya.

Vifo vinavyoepukika

A Picture and its Story: I would rather die than go back, Moroccan migrant boy tells Spanish soldier
Mhamiaji wa Kimorocco akishikiliwa baada ya kuogelea kuingia Ceuta, mamlaka ya Uhispania.Picha: Jon Nazca/REUTERS

Ripoti hiyo ilisema watu hufa wakiwa katikati ya mkondo wa bahari kwa sababu ama waokowaji hufika wakiwa wamechelewa ama hawafiki kabisa.

"Walinzi wa jeshi la wanamaji la Libya ndio wanaofanya sehemu kubwa ya kazi ya uokowaji kwa niaba ya Umoja wa Ulaya kwenye eneo la bahari la kimataifa," ilisema ripoti hiyo, lakini ikionya kuwa walinzi hao huwarejesha Libya wahamiaji wanaofanikiwa kuwaokowa "jambo ambalo si salama pia kwa waliookolewa kutokana na matukio kadhaa ya uvunjaji wa wazi wa haki zao."

Katika mwaka 2020, wahamiaji 10,352 walizuiliwa njiani na kurejeshwa Libya, huku mwaka 2019, waliozuiliwa na kurejeshwa wakiwa 8,403.

Bachelet aliutaka Umoja wa Ulaya kuanzisha njia nyingi na za halali kwa wahamiaji kuingia barani Ulaya.

"Tunaweza sote kukubaliana kwamba hakuna mtu hata mmoja anayepaswa kujiona analazimika kubahatisha maisha yake ama ya familia yake kwenye mashua mbovu katika jitihada za kusaka usalama na hishima ya maisha yake," alisema kamishna huyo, akisisitiza kwamba "jibu haliwezi kuwazuwia watu wasiondoke kutokea Libya ama kuzifanya safari zao kuwa za kuogofya na za fadhaa."