1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa walaani matumizi ya silaha nzito Libya

Sylvia Mwehozi
17 Aprili 2019

Ujumbe wa usaidizi wa Umoja wa Mataifa Libya umelaani ongezeko la matumizi ya silaha nzito na mashambulizi holela dhidi ya makazi ya watu, shule na miundombinu na kutaka huduma za dharura kuwafikia raia waliokwama

https://p.dw.com/p/3GwDk
Auseinandersetzungen zwischen Haftars Streitkräften und der libyschen Regierung in Tripolis
Picha: Reuters/E. Al-Fetori

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM, idadi ya watu wasio na makazi ndani na nje ya mji wa Tripoli hivi sasa inakaribia 20,000. Zaidi ya watu 2,400 walikimbia makazi yao katika kipindi cha masaa 24 pekee.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujaric, amewaambia waandishi wa habari jijini New York kwamba familia nyingi zinazokimbia maeneo yaliyo na machafuko zinaelekea katikati mwa Tripoli na maeneo ya karibu, lakini takribani watu 14,000 wasio na makazi wametafuta hifadhi nje ya mji huo mkuu katika maeneo ya Tajoura, Al Maya, Ain Zara na Tarhouna.

"Mjumbe maalum wa katibu mkuu anafanya kazi na serikali na pande zote Libya, sambamba na wawakilishi wa kimataifa kujaribu kusitisha mapigano, na kusonga mbele na mchakato wa kisiasa. Ninafikiri Bw. Salame alikuwa wazi kwamba mkutano wa kitaifa haukufutwa. Anataka kuendelea nao lakini hilo halitawezekana ikiwa watu wanafyatuliana risasi na kuwaua raia, alisema Dujaric. 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana lilianza kujadili azimio lililoandaliwa na Uingereza la kutaka kusitishwa mapigano nchini Libya, baada ya majeshi tiifu ya kamanda Khalifa Haftar kuanzisha mashambulizi mjini Tripoli.

Libyen UN-Sondergesandter Ghassan Salame
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Libya Ghassan SalamePicha: picture-alliance/Photoshot

Azimio hilo linaonya kuwa mashambulizi ya jeshi la Haftar yanatishia usalama na mustakabali wa mazungumzo ya kisiasa yanayoratibiwa na Umoja wa Mataifa, sambamba na upatikanaji wa suluhisho la kisiasa la mgogoro huo. Baraza hilo pia limezitolea wito pande zote zinazohusika nchini Libya, kuheshimu usitishaji mapigano na kushiriki katika mazungumzo ya kuhakikisha hali ya usalama inarejea kote nchini Libya.

Mapigano mapya nchini Libya yalizuka kiasi wiki mbili zilizopita wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres, baada ya kiongozi wa vikosi vya mashariki Jenerali Khalifa Haftar kuanzisha operesheni ya kuchukua udhibiti wa mji mkuu Tripoli na kukabiliana na upinzani wa vikosi vya serikali inayotambuliwa kimataifa.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa kuwahudumia wakimbizi, UNHCR, jana liliwahamisha wakimbizi wengine 150 waliokuwa wakishikiliwa katika kituo cha Abu Selim kusini mwa Tripoli. Kituo hicho ni miongoni mwa vituo kadhaa nchini Libya ambavyo vimeathirika tangu mapigano yalipozuka. Zaidi ya wakimbizi na wahamiaji 2700 bado wanashikiliwa na kukwama katika maeneo ambako mapigano yanaendelea.