1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waonya kukithiri kwa matamshi ya chuki DRC

8 Januari 2024

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake siku ya Jumapili kuhusu kuongezeka kwa mvutano wa kikabila na miito ya vurugu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4axS0
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi akiwa kwenye kampeni za uchaguzi mjini Kinshasa:18.12.2023Picha: AFP

Afisa wa ngazi ya juu anayehusika na masuala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake siku ya Jumapili kuhusu kuongezeka kwa mvutano wa kikabila na wito wa vurugu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufuatia uchaguzi wenye utata.     

Ucheleweshaji mkubwa, ukiritimba na vurugu viliutia doa uchaguzi uliofanyika Desemba 20 ili kumchagua rais, wabunge wa kitaifa na mikoa, madiwani na viongozi wa serikali za mitaa.    

Kufikia sasa tume ya uchaguzi imetangaza pekee matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyompa ushindi wa kishindo rais aliye madarakani na anayewania muhula wa pili Felix Tshisekedi, ushindi ambao umetupiliwa mbali na upinzani wakiutaja kuwa wa udanganyifu.

 Soma pia: Tume ya uchaguzi Kongo yafuta matokeo ya wagombea ubunge

Wagombea Urais katika uchaguzi wa mwaka 2023 nchini Kongo(DRC):  Moise Katumbi, Martin Fayulu und Felix Tshisekedi
Wagombea wakuu wa Urais katika uchaguzi wa Desemba 20, 2023 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo: Moise Katumbi (kushoto), Martin Fayulu (katikati) na Felix Tshisekedi (kulia)

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Volker Turk amesema: "Nina wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka kwa matamshi ya chuki yenye misingi ya kikabila na uchochezi wa  ghasia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo."

Turk amesema miito ya kufanyika ghasia baada ya uchaguzi huo imekuwa ikitolewa hasa katika mikoa ya Kasai na Katanga pamoja na majimbo ya mashariki ya Kivu Kaskazini na Kusini, ambayo yamekumbwa na vurugu za makundi yenye silaha na mauaji ya kikabila kwa miongo kadhaa.      

Tshisekedi anatokea katika mkoa wa Kasai huku aliyekuwa mpinzani wake mkubwa katika uchaguzi huo Moise Katumbi, akiwa ni kutoka Katanga.  

Tishio kwa usalama wa kikanda

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk
Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk akizungumza na waandishi wa habari mjini Cairo, nchini Misri: 08.11.2023 kuhusu mzozo wa Gaza.Picha: KHALED DESOUKI/AFP

Turk amesisitiza kuwa: "Maneno ya chuki, yasiyo na utu na ya uchochezi hayafai na yanaweza tu kuongeza mvutano na vurugu nchini Kongo, pamoja na kuhatarisha usalama wa kikanda."

Amezitaka mamlaka "kuchunguza kwa kina na kwa uwazi ripoti zote za matamshi ya chuki na uchochezi wa ghasia na kuwawajibisha wale wote watakaobainika kuhusika".

 Soma pia:   Maaskofu waomba mwanga kuhusu kasoro za uchaguzi Kongo

Mivutano inayohusiana na uchaguzi imekuwa ikishuhudiwa mara kadhaa nchini Kongo ambayo ina historia ya utawala wa kimabavu na mapinduzi ya serikali.

Karibu makabila 250 yanaishi katika nchi hiyo kubwa ya Afrika ya Kati yenye utajiri mkubwa wa madini lakini idadi ndogo kabisa ya watu wake karibu milioni 100 ndio hunufaika na utajiri wa taifa lao.

(Chanzo:AFPE)