1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Majenerali wa Sudan watakiwa wahakikishe usalama wa misaada

Josephat Charo
4 Mei 2023

Kwa mara nyingine tena Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kusitishwa mapigano, akisema nchi hiyo haiwezi kuendeleza uharibifu unaoshuhudiwa katika wakati huu.

https://p.dw.com/p/4Qrzh
UN-Nothilfekoordinator Griffiths
Picha: Martial Trezzini/KEYSTONE/dpa/picture alliance

Umoja wa Mataifa unawashinikiza majenerali wa pande zinazohasimiana Sudan wahakikishe usalama kwa misafara ya magari ya misaada ya kiutu baada ya malori sita ya misaada kuporwa huku mashambulizi ya kutokea angani yakivuruga mkataba wa usitishaji mapigano. Mkuu wa uratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths amesema watahitaji kuwa na muafaka katika ngazi ya juu kabisa na hadharani ili kuruhusu safari za wafanyakazi wa misaada na usambazaji wa mahitaji muhimu.

Griffiths alikuwa akizungumza katika mji wa bandari wa Port Sudan katika pwani ya bahari ya shamu, ambako watu wengi wamekimbia baada ya wiki mbili za mapigano makali kati ya jeshi la Sudan na kikosi cha wanamgambo cha RSF. Ziara ya Griffiths Port Sudan ililenga kuratibu operesheni kubwa ya utoaji misaada ya kibinadamu ambapo baadaye alielekea Jeddah, Saudi Arabia. Ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu akiwa Jeddah kwamba ana matumaini atakutana ana kwa ana na pande zinazohasimiana Sudan katika siku mbili au tatu zijazo wamhakikishie usalama wa maafisa na misafara ya misaada. Mkutano huo huenda ukafanyika mjini Khartoum au eneo lengine.

Jordanien Amman | ICRC-Mitglieder bereiten humanitäre Hilfsgüter für den Sudan vor
Majenerali wa Sudan watakiwa kulinda misafara ya misaadaPicha: ICRC/AFP

Mashambulizi ya kutokea angani yalirindima mjini Khartoum na miji iliyo karibu ya Omdurman na Bahri jana Jumatano, licha ya pande zinazopigana kuafikiana kurefusha mfulululizo wa mikataba dhaifu ya usitishaji mapigano kwa siku nyingine saba kuanzia leo Alhamisi.

Hakuna mazungumzo ya ana kwa ana na wanamgambo

Huku wapatanishi wa kimataifa wakishinikiza mazungumzo ya amani yafanyike, jeshi la Sudan limesema litamtuma mjumbe kwa mazungumzo na viongozi wa Sudan Kusini, Kenya na Djibouti. Mjumbe wa Mkuu wa majeshi ya Sudan Jenerali Abdel Fattah al Burhan, Dafallah Alhaj amesema mjii Cairo, Misri kwamba jeshi limeyakubali mazungumzo lakini hakutafanyika mazungumzo ya ana kwa ana na wanamgambo wa RSF. Alhaj amesema mawasiliano kati ya pande hizo mbili yatafanyika kupitia wapatanishi.

Awali katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliitaka jumuiya ya kimatifia iwaambie jenerali al Burhan na kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo, kwamba hali ya sasa ya Sudan haikubaliki. Akizungumza akiwa mjini Nairobi, Kenya, Guterres alitaka pia majenerali hao washinikizwe waache mapigano, waanze mdahalo na waruhusu kipindi cha mpito kuelekea serikali ya kiraia.

Sudan iilitangaza Jumanne kwamba watu 550 wameuliwa na wengine 4,926 wamejeruhiwa tangu vita vilipozuka nchini humo Aprili 15. Umoja wa Mataifa unasema watu takriban 100,000 wamekimbia wakiwa na chakula kichache au maji hadi katika nchi nchi jirani.

Msaada umekwama Sudan, taifa lenye idadi ya wakazi milioni 46 ambako theluthi moja walikuwa tayari wakitegemea msaada wa chakula kabla machafuko kuzuka.

Griffiths amesema amefahamishwa na shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP kwamba malori yao sita yaliyokuwa njiani kuelekea eneo la magharibi la Sudan, Darfur, yaliporwa licha ya kuhakikishiwa usalama na ulinzi. Hakuna kauli yoyote iliyotolewa mara moja na shirika la WFP.

(rtre, afpe)