1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya na mzozo wa Kongo

31 Oktoba 2008

Ufaransa yapendekeza vikosi vya Ulaya kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

https://p.dw.com/p/FlIU

Umoja wa Ulaya unazingatia vipi kuwasaidia wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na kuutatua ugomvi uliozuka. Ufaransa ikiwa mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya, itaamua hadi mwishoni mwa wiki hii ijiungea katika mazungumzo ya kuamua iwapo na kwa namna gani, Umoja wa Ulaya ujiingize kijeshi nchini kongo.

Hatua ya kwanza ilichukuliwa na waziri wa nje wa Ufaransa ,Bernard Kuschner hapo jana ,lakini ikapingwa hasa na Ujerumani.Matamshi yake kuwa Umoja wa Ulaya utume majeshi yake Kongo ili kuviimarisha vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kuhifadhi amani viliopo huko,yalipokewa kwa shingo upande na serikali ya Ujerumani mjini Berlin.

Ilikua Ubelgiji,mkoloni wa zamani wa Kongo, alieitikia pendekezo hilo.Waziri wake wa mambo ya nje Karel De Gucht akaipokea pasi hiyo aliyotupiwa na waziri wa nje wa Ufaransa.

"Tunalizingatia hivi sasa kwa kadiri gani ujiingizaji kijeshi wa vikosi vya Ulaya wawezekana."

Alisema waziri wa nje wa Ubelgiji. Kuschner amependekeza kuwa UU ungeweza kupeleka nchini Kongo kikosi cha askari 1500 ambacho mnamo muda wa wiki mbili kingeweza kutumika popote pale humo nchini.Kuna vikosi mbali mbali,vilivyokaa tayari kutumika lakini, ni vikosi 2 tu.Hivi ni vikosi vya Uingereza na vile kati ya Ujerumani na Ufaransa ,ambamo pia askari wa Ubelgiji,Luxemburg na wa Spian wamejiunga navyo.

Ikiwa mtu atalizingatia shauri la waziri wa nje wa Ufaransa kikamilifu, basi askari wa Ujerumani nao watapelekwa nao mashariki mwa kongo.

Hivi sasa lakini Bw.Kuschner, anasisitiza kwamba swali sio vikosi vya UU kwenda kupigana bega kwa bega na vile vya Umoja wa Mataifa,bali zaidi jukumu lao liwe kusaidia shughuli za uokozi.Mfano kugawa shehena za misaada .Ubelgiji lakini ,yaonesha iko hata tayari kujiingiza .Kwani, Kongo iko moyoni kabisa mwa Ubelgiji, ilikua koloni lake.

Miaka 2 nyuma , Umoja wa Ulaya ulituma kikosi cha askari 780 kusimamia uchaguzi wa kwanza huru nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Ilikua Ufaransa iliotoa shauri hilo na baada ya mvutano na patashika ndefu na Ujerumani, ilifaulu .Ujumbe huo ingawa ulifanikiwa, lakini mjini Berlin hamu ya kujitosa tena katika majanga ya Afrika haipo kabisa.

Umoja wa Ulaya hapo jana ulijitolea msaada wake wa kwanza wa dharura wa Euro milioni 4 kwa wakimbizi.Kamishna wa misaada ya maendeleo wa Umoja wa Ulaya, Louis Michel,pia mbelgiji hivi sasa yuko nchini Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo ili kujionea hali ya mambo kwa macho yake. Anapendekeza suluhisho la mazungumzo la mzozo uliozuka.

Kwa hali inavyoonekana ,wafaransa wamevinjari hata kutuma Kongo wanajeshi wa Umoja wa Ulaya .Yadhihirika Ujerumani haitaweza nayo kutoitikia mwito huo.