1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya na wimbi la wakimbizi kutoka Afrika

Oummilkheir13 Juni 2007

Maombi ya Malta ya kugawana mzigo wa wakimbizi yamepingwa lakini mipango mengine inadurusiwa

https://p.dw.com/p/CHka
Picha: AP

Umoja wa Ulaya unajibu tatizo la wimbi jipya la wakimbizi katika eneo la bahari ya Mediterenia kwa kutoa fedha zaidi na kuzidisha doria.Maombi ya Malta ya kugawana ipasavyo miongoni mwa mataifa 27 ya Umoja wa ulaya,wahamiaji wa kiafrika waliookolewa baharini,yamepingwa na mawaziri wa mambo ya ndani walipokutana jana mjini Luxembourg.Waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu ya Ujerumani Wolfgang Schäuble amesema wazi kabisa jambo hilo haliwezekani kabisa kwa sasa.Siku za mbele ufumbuzi wa haki unaweza kupatikana.Wakati huo huo bwana Schäuble akashadidia mshikamano wa nchi yake kwa Umoja wa Ulaya.Malta haitaachwa mkono-amesema.

“Aibu kwa Umoja wa Ulaya”- matamshi hayo yalitolewa mwishoni mwa mwezi uliopita na kamishna wa Umoja wa ulaya Franco Frattini,pale mashua zilizosheheni wakimbizi wa kiafrika zilipokwama katika wavu wa samaki kwa muda wa siku tatu-kwasababu Libya na Malta zilishindwa kufikia makubaliano ya kuwaokoa wakimbizi hao.Ilikua meli ya kitaliana iliyokuja kuwaokoa hatimae wakimbizi hao. Kwamba kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi, hafanyi kitu si jambo la kustaajabisha,lakini kwamba Malta,mwanachama wa Umoja wa Ulaya inafumba macho-hapo hakuna jengine la kusema isipokua - aibu !

Na ni aibu kweli kweli tena kwa Umoja wa Ulaya .Ni sawa pale kisiwa hicho kidogo cha bahari ya kati kinapohoji kwamba hakina tena uwezo wa kuwapokea wahamiaji zaidi. Malta imeshauri pia wakimbizi hao walioingia kwa mashua watawanywe katika nchi nyengine za Umoja wa ulaya.Madai hayo yanaingia akilini lakini katika suala hilo mshikamo miongoni mwa nchi wanachama wa umoja wa mataifa ni kitu adimu.

Hapo kila mmoja hakawii kukumbusha,tokea hapo nchi yake inazongwa na wakimbizi wa kutoka Ulaya ya mashariki-kama vile ambavyo Ujerumani daima imekua ikisema.

Misaada ya fedha kutoka makasha ya umoja wa ulaya itatolewa bila ya shida,ikiwa wataepukana na shinikizo la kuwapokea wakimbizi waliokata tama kutoka Afrika,wanaosaka kazi na riziki.Na dhahiri ni kwamba nchi za Umoja wa ulaya haziwezi kuwapokea mamilioni ya waafrika wenye njaa kwasababu wazungu wenyewe wamezongwa na juhudi za kuileta pamoja jamii yao.Na dhahiri pia ni kwamba hawawezi kuwaacha wakimbizi hao wazame katika bahari ya mediterenia.Kambi za mapokezi nchini Italy au kusini mwa Hispania,kugawana sawa wakimbizi au hatua yoyote ile nyengine ni bora kuliko hali namna ilivyo hivi sasa.

Kutokana na shinikizo la halmashauri kuu ya umoja wa ulaya,kunaandaliwa mpango ambapo nchi za umoja wa ulaya zitajikuta zikiacha mwanya kidogo katika mlango wa ngome yao.

Siku za mbele itaruhusiwa kuwaajiri mashambani au katika shughuli za ujenzi wafanyakazi wa muda kutoka Afrika.Makubaliano yatabidi yafikiwe pamoja na nchi wafanyakazi hao wanakotokea kwanamna ambayo viza zao zikimalizika wataruhusiwa kurejea nyumbani.Nchi gani ya Ulaya itajifungamanisha na mpango huo na waafrika wangapi watapata fursa ya kufanya kazi hizo-hakuna bado ajuae.

Pengine ni watu mia kadhaa tuu-na japo kama huo si ufumbuzi-mradi ni ishara ya matumaini.