1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya una msimamo wa pamoja kuhusu Brexit

Sekione Kitojo
27 Aprili 2017

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliamua kuvunja matumaini ya Uingereza kwamba kujitoa kwao katika Umoja wa Ulaya kutakuwa  na athari ndogo katika mahusiano, haki na vivutio ambavyo hivi sasa inavyo.

https://p.dw.com/p/2c1m0
Angela Merkel Regierungserklärung Berlin
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/H.Hanschke

Hayo  yamesemwa  leo(27.04.2017)  na  kansela Merkel  bungeni  wakati akilihutubia  bunge  kabla  ya mkutano  wa  viongozi  wa mataifa 27  yaliyobakia katika  Umoja  huo  mjini  Brussels siku  ya  Jumamosi.

Mataifa 27  ya  Umoja  wa  Ulaya  yanaingia  katika mchakato  wa  miaka  miwili  wa  majadiliano  ya  talaka  na Uingereza  yakiwa  pamoja  zaidi  mara  hii, na  kwamba kuna  msimamo  wa  pamoja  zaidi  kuhusiana  na muongozo  wa  majadiliano  hayo  ambao  unapaswa kuidhinishwa  katika  mkutano  wa  Jumamosi.

Großbritannien Michel Barnier
Mkuu wa ujumbe wa majadiliano wa Umoja wa ulaya Michel BanierPicha: picture-alliance/Zumapress/T. Akmen

Mara  kadhaa  yakiwa na  misimamo  inayotofautiana kuhusiana  na  masuala  muhimu  kuanzia  wakimbizi  hadi katika  mzozo  wa  kifedha, mataifa  ya  Umoja  wa  Ulaya yamesema  hakuna  masuala  makubwa  ambayo yatawashughulisha  viongozi  hao katika  mkutano  huo  wa mwishoni  mwa  juma.

Mwenyekiti  wa  tume  ya  majadiliano  Michel Banier , amesema  kwamba  "tuko tayari, tuko  tayari" kuingia katika  majadiliano , wakati  akiingia  katika  mkutano  mjini Luxembourg. Mara  muongozo  utakapoidhinishwa  siku  ya Jumamosi, makao  makuu  ya  Umoja  wa  Ulaya utayaingiza  katika  muongozo  wa  majadiliano  kwa  ajili ya  Banier  hali  ambayo  inatakiwa  kuwa  tayari  ifikapo Mei 22.

Festakt zum 50. Todestag von Konrad Adenauer
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture alliance/dpa/M.Gambarini

Wakati  wa  kuwa  pamoja

Mazungumzo  yanatarajiwa  kuanza  baada  ya  uchaguzi nchini  Uingereza  utakaofanyika  Juni 8.

"Mkutano  huo  ulikuwa muhimu  kwa  dhana  kwamba  ni ishara  muhimu  ya  kuaminiana, umoja  na  msimamo  wa pamoja  kwa  mataifa  hayo  27," amesema  naibu  waziri mkuu  wa  Malta Louis Grech , aliyekuwa  mwenyekiti  wa mkutano  wa  mawaziri.

"Tumeweka  wazi  katika  muongozo  kwamba  soko la pamoja  halitagawanyika na  kwamba  hakutakuwa  na kuchagua chagua. Nafikiri  hilo  liko  wazi  na  linaeleweka ndani  ya  utaratibu  wa  muongozo. Iwapo  wanaota ama kutoota , sitakwenda upande  huo. Mimi  si  mfumbuzi wa siri  kujua  kama wana  mawazo ya  kufikirika. Kwa  hiyo nafikiri  kadri  muda  unavyokwenda  tutafahamu kwa hakika  ni  msimamo  gani  kuhusiana  na  soko  la  pamoja kuihusu Uingereza."

Brexit-Hauptakteure - Jean-Claude Juncker
Rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude JunckerPicha: Getty Images/C. Court

Wakati  bado  Umoja  wa  Ulaya  unaiangalia  Uingereza kama mshirika  wa  karibu , kansela  wa  Ujerumani  Angela Merkel  alisema  mara  talaka  itakapotolewa  na  nchi  hiyo kujiondoa  kutoka  Umoja  huo  nchi  hiyo  itakuwa  nje  na kamwe haitakuwa  na  haki  sawa  ama  kuwa  katika  nafasi bora  kuliko  nchi  mwanachama  wa  Umoja  huo. " Amesema  wanachama  wote 27 wa  Umoja  wa  Ulaya  na taasisi  za  Ulaya  wanakubaliana  kwa  hilo."

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape

Mhariri: Yusuf , Saumu