1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wachunguza soko la vifaa vya matibabu China

24 Aprili 2024

Umoja wa Ulaya umeanzisha uchunguzi kuhusu soko la China la vifaa vya matibabu ,hatua ambayo imeifanya China kuutuhumu Umoja huo kwamba unajiingiza katika hatua za kulinda soko lake dhidi ya makampuni ya China.

https://p.dw.com/p/4f9A9
Wang Wenbin
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China, Wang WenbinPicha: Mark Schiefelbein/AP

Jarida rasmi la kiutawala la Umoja wa Ulaya likitangaza uchunguzi huo, limeorodhesha njia ambazo huenda zinatumika katika masoko hayo ikiwa ni pamoja na sera ya manunuzi ya China. 

Aidha jarida hilo limetaja wasiwasi kwamba huenda China imeweka vikwazo vya uagizaji bidhaa kutoka nje na kuweka masharti ya kusababisha zabuni za chini kwa njia isiyo ya kawaida ambazo makampuni yanayolenga kutengeneza faida hayawezi kuhimili. 

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China, Wang Wenbin, amejibu kwa kusema kwamba uchunguzi huo "utaharibu sura ya Umoja wa Ulaya" 

Wenbin amesema ulimwengu unashuhudia hatua kwa hatua jinsi umoja huo unavyoelekea kwenye ulinzi, akitoa wito kwa Brussels kuacha kutumia kisingizio kukandamiza na kuzuia biashara ya China bila misingi.