1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wafikia makubaliano na Uturuki

18 Machi 2016

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameidhinisha makubaliano na Uturuki mjini Brussels kudhibiti mzozo wa wahamiaji na hivi sasa inasubiriwa idhini kutoka kwa Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu.

https://p.dw.com/p/1IFxu
Ahmet Davutoglu Waziri Mkuu wa Uturuki na viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels. (18.03.2016)
Ahmet Davutoglu Waziri Mkuu wa Uturuki na viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels. (18.03.2016)Picha: picture-alliance/dpa/O.Hoslet

Waziri Mkuu wa Finland Juha Sipila ameandika katika mtandao wake wa Twitter kwamba makubaliano hayo na Uturuki yamefikiwa wakati viongozi wa nchi wanachama 28 wa Umoja wa Ulaya walipokutana kujadili makubaliano hayo.

Afisa mwengine wa Umoja wa Ulaya aliyekataa kutajwa jina amethibitisha kufikiwa kwa makubalino hayo na kimsigi sasa inasubiriwa mazungumzo ya mwisho na waziri mkuu wa Uturuki.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na Uturuki leo walikuwa katika mazungumzo magumu wakati Umoja wa Ulaya ikitaka kuwarudisha Uturuki maelfu ya wahamiaji na kupunguza shinikizo la hali ya dharura ya kibinaadamu ambalo linazidi kuugawa umoja huo.

Msimamo mgumu wa Uturuki

Akionyesha msimamo mgumu na mapema Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu amesema wasi wasi mkuu wa serikali yake ni hatima ya takriban wakimbizi milioni 3 wa Syria walioko katika ardhi yake.Wakati huo huo waziri mkuu huyo anatarajia Umoja wa Ulaya iridhie hatua zisizo kifani za kuisogeza karibu zaidi na Umoja wa Ulaya nchi hiyo jirani.

Waziri Mkuu wa Uturuiki Ahmet Davutoglu mjini Brussels. (18.03.2016)
Waziri Mkuu wa Uturuiki Ahmet Davutoglu mjini Brussels. (18.03.2016)Picha: picture-alliance/dpa/S. Lecocq

Davutoglu amesema "Kwetu sisi,kwa Uturuki suala wakimbizi sio suala la kupatana bali ni suala la maadili ni suala zima la kibinaadamu halikadhalika ni suala la maadili la Ulaya.Uturuki imepokea wakimbizi milioni 2.7 bila ya msaada wa maana kutoka popote pale."

Davutoglu amesema anataraji mbali ya kuwasaidia wakimbizi makubaliano hayo pia yataimarisha uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Uturuki.

Kupunguzia mzigo Ugiriki

Wakati wahamiaji milioni moja wakiwa wamewasili barani Ulaya katika kipindi cha mwaka mmoja viongozi wa Umoja wa Ulaya wako mbioni kutaka kufikiwa makubaliano na Uturuki na kusuluhisha mgawanyiko mkubwa miongoni mwa nchi wanachama 28 wa Umoja wa Ulaya wakati huo huo ikipunguza shinikizo kwa Ugiriki ambayo imebeba mzigo mkubwa wa kuwasili kwa wahamiaji wapya.

Mkutano wa Kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki Brussels. (18.03.2016)
Mkutano wa Kilele kati ya Umoja wa Ulaya na Uturuki Brussels. (18.03.2016)Picha: Reuters/S. de Sakutin

Mazingira ya wahamiaji nchini Ugiriki na katika kambi ya Idomeni yametajwa kuwa yasio ya kuvumulika na serikali hapo jana.Waziri wa mambo ya ndani wa Ugiriki Panagiotis Kouroumplis wakati wa ziara katika kambi hiyo ameulinganisha mji huo wa mahema sawa na kambi ya mateso na kulaumu kuteseka kwa wahamiaji kumetokana na sera za kufunga mipaka za baadhi ya mataifa ya Umoja wa Ulaya.

Zaidi wahamiaji 46,000 wamenasa nchini Ugiriki baada ya Austria na nchi mbali mbali za Balkan kuzuwiya kuruhusu wakimbizi walioingia Ugiriki kutoka Uturuki kuendelea na safari kuelekea katika nchi zenye neema barani Ulaya.

Chini ya makubaliano hayo Umoja wa Ulaya utalipia wahamiaji wapya wanaowasili Ugiriki ambao hawastahiki kupatiwa hifadhi kurudi Uturuki. Kwa kila Msyria mmoja anayerejeshwa,Umoja wa Ulaya itakubali kumpokea mkimbizi mmoja wa Syria na kufikia hadi watu 72,000 watakaogawanywa katika mataifa ya Ulaya.

Mbali na kuregeza masharti ya visa Umoja wa Ulaya pia utaipatia Uturuki msaada wa hadi euro bilioni sita pamoja na kuharakisha mazungumzo ya Uturuki kujiunga na umoja huo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri :Yusuf Saumu