1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waipunguzia Kenya fedha

Yusra Buwayhid
31 Julai 2019

Umoja wa Ulaya umepunguza kwa nusu, kiwango cha fedha zilizotengewa Kenya katika mapambano yake dhidi ya kundi la Alshabaab nchini Somalia.

https://p.dw.com/p/3N4QB
Somalia kenianische Soldaten der Afrikanischen Union
Picha: Getty Images/AFP/AU-UN Ist Photo/S. Price

Umoja wa Ulaya na washirika wake wamekipunguza kwa nusu kiwango cha fedha zilizotengewa Kenya kwa mchango wake katika  mapambano dhidi ya Al Shabaab nchini Somalia.

Takwimu mpya zinaashiria kuwa serikali ya Kenya ilirejeshewa shilingi bilioni 4.3 kwa mwaka wa fedha uliokamilika mwezi uliopita wa Juni ambazo ni nusu ya kile ilichotarajia. Kwa mwaka huu mpya wa fedha Kenya inasubiria shilingi bilioni 5 pekee.

Hata hivyo, Umoja wa Ulaya umeahidi kuendelea kuunga mkono ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM kwenye harakati zake za mwaka wa fedha wa 2019/20.

Mchango wa Umoja wa Ulaya unagharamia malipo ya vikosi na jeshi, wahudumu na operesheni za kila siku. Kwa upande wa pili afisi ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi nchini Somalia UNSOS inachangia nyenzo kwenye operesheni za vikosi vya AMISOM na wanajeshi wa Somalia. Hata hivyo Umoja wa Mataifa unakabiliana na hali ngumu ya fedha kwa sasa.

Kulingana na ratiba, azma ya vikosi vya AMISOM na washirika wake ni kulikabidhi jeshi la kitaifa la Somalia majukumu ya kulinda usalama ifikapo mwaka 2021.

Ujumbe wa umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM unawaleta pamoja wanajeshi kutokea mataifa 6 ya kiafrika kupambana na wapiganaji wa Al Shabaab.

Kulingana na takwimu, kila mwanajeshi anayehudumu Somalia anapokea dola 1028 kwa mwezi.