1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wakubali vikwazo kwa Lukashenko

12 Oktoba 2020

Umoja wa Ulaya Jumatatu umekubali kumuwekea vikwazo kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko, wakati jumuiya hiyo ikitafuta njia za kuongeza shinikizo dhidi ya harakati za utawala wake za kuwaandama waandamanaji.

https://p.dw.com/p/3jodc
Weißrussland | Alexander Lukaschenko
Picha: Maxim Guchek/BelTA/TASS/dpa/picture-alliance

Kutoka Luxembourg ambako unafanyika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje ya Umoja wa Ulaya, vyanzo viwili vya kidiplomasia vimeeleza kwamba mawaziri 27 wa nchi 27 za Umoja wa Ulaya wamekubaliana kwamba jina la Lukashenko lijumuishwe kwenye orodha ya maafisa wake 40 wa Belarus ambao tayari wameshawekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya.

Maafisa hao 40 wa serikali ya Belarus tayari wanakabiliwa na vikwazo vya usafiri na mali zao kuzuiwa na wanalaumiwa kwa kuhusika na wizi au undanganyifu uliotokea kwenye uchaguzi mnamo mwezi Agosti ambao ulitowa matokeo yaliyomrudisha madarakani rais Lukashenko.

Lakini pia maafisa hao wanatuhumiwa kuhusika na harakati za kikatili za kuwaandama waandamanaji waliojitokeza katika maandamano makubwa ya uma yaliyoikumba nchi hiyo tangu ulipofanyika uchaguzi.

Umefikia wakati wa kutanua vikwazo kwa Belarus

Umoja wa Ulaya ulijizuia kumuadhibu Lukashenko binafsi jumuiya hiyo ikitarajiwa kwamba itamshawishi kuingia kwenye meza ya mazungumzo na upinzani ili kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo wa kisiasa.

Deutschland I Fragestunde BT - Heiko Maas -  Bundesregierung
Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani heiko MaasPicha: Uwe Koch/Eibner-Pressefoto/picture-alliance

Lakini hatua mpya ya kuwaandama waandamanaji katika mji mkuu Minsk Jumapili ambapo polisi walionekana wakitumia mabomba ya maji na magureneti ya kuwatawanya watu katika maandamano hayo na kuwakamata mamia ya waandamanaji, imechochea kufanyika mabadiliko hayo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas wakati anaingia kwenye mkutano huo wa Luxembourg alisema umefika muda wa kutanua orodha ya vikwazo ikiwemo kumjumuisha kiongozi huyo wa Belarus.

''Tunapaswa kukubali kwamba tangu mkutano wetu wa mwisho hakuna kilichoimarika.Utawala wa Lukashenko unaendelea kufanya vurugu,bado kuna ukamataji wa waandamanaji wanaoandamana kwa amani. Na hiyo ndio sababu ya kwanini tunapaswa kufikiria hatua za kuchukua. Napendekeza kufungua njia ya vikwazo vipya na Lukashenko lazima awe miongoni mwa watakaokuwemo kwenye orodha hiyo," alisema Heiko Maas. 

Orodha ya vikwazo vipya itashughulikiwa kwa kina na idara za sheria za Umoja wa Ulaya

Kinachotakiwa kufahamika hapa ni kwamba Umoja wa Ulaya umekataa kuyatambua matokeo ya uchaguzi wa Belarus wa Agosti 9 na umesema haumtambui Lukashenko kama kiongozi halali wa nchi hiyo.

EU-Ukraine-Gipfel in Brüssel
bendera ya Umoja wa Ulaya ikipepea katika makao makuu BrusselsPicha: Ye Pingfan/Photoshot/picture alliance

Sasa baada ya kupata idhini hiyo ya kisiasa ya mawaziri hao, orodha ya vikwazo vipya itashughulikiwa kwa kina na idara za sheria za Umoja wa Ulaya kabla ya kuanza kutekelezwa.

Juu ya hilo mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya walizungumzia pia pendekezo la pamoja lililotolewa na Ufarnsa na Ujerumani la vikwazo kuhusiana na suala la kutiliwa sumu kiongozi wa upinzani wa Urusi Alexei Navalny.

Mawaziri hao wameongeza vikwazo chini ya utaratibu maalum wa vikwazo vya umoja wa Ulaya vya silaha za sumu,na katika utaratibu huo tayari wameorodheshwa maafisa wanne wa Urusi waliotuhumiwa kuhusika katika kisa cha mwanzo kabisa cha kutumiwa sumu ya Novichok,dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi aliyekuwa amekimbilia Uingereza.

Kwa maana hiyo vikwazo vyoyote vitakavyotolewa kuhusiana na kisa cha Alexei Navalny vitatolewa chini ya mpango huo. Mbali na hayo mkutano wa Umoja wa Ulaya pia utamulikia mazungumzo kati ya Serbia na Kosovo yanayosimamiwa na Jumuiya hiyo sambamba na mgogoro unaoshika kasi wa jimbo la Nagorno Karabakh.