1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN kupiga kura dhidi ya zana za kemikali Syria

24 Februari 2017

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria  Staffan de Mistura ameyataka makundi yanayotofautiana katika mazungumzo ya taifa hilo linalokumbwa na mzozo watafute mwafaka utakaopelekea kufikia kikomo kwa mapigano hayo.

https://p.dw.com/p/2YBs5
Schweiz Genf Staffan de Mistura
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de MisturaPicha: Reuters/P. Albouy

Mazungumzo kuhusu mapigano hayo yaliyodumu kwa kipindi cha miaka sita, yanatarajiwa kudumu kwa siku nzima Ijumaa.

Kwenye ufunguzi wa mazungumzo hayo Alhamis huko Geneva, Uswizi, de Mistura alisema hatarajii miujiza katika kupatikana kwa suluhisho na akaonya pia kutakuwa na malipo iwapo suluhu halitopatikana kwa mara nyengine.

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa alisema, "hili ni jukumu letu, jukumu letu la kuhakikisha kwamba kizazi kijacho cha watoto wa Syria, hakishuhudii kipindi kirefu cha mapigano na umwagikaji damu."

"Kwasababu kuna maelfu na maelfu ya kina mama na wasichana wanaotarajia kwamba hili suala litakuwa mojawapo ya manufaa ya mazungumzo yoyote, na siwezi kulikataa hilo, kwasababu nahisi jinsi wanavyohisi" alisema de Mistura.

HNC inataka iwe mwakilishi wa pekee

De Mistura amesema atafanya mazungumzo Ijumaa kwa mujibu wa mwongozo uliopo. Upande mkuu wa upinzani HNC umesema unataka kukutana na serikali moja kwa moja, ila makundi mengine mawili ya upinzani yaliyo na makao yake Moscow na Cairo na ambayo kwa sasa yako huko Geneva yamesema pia kwamba yanataka kuwepo kwenye mazungumzo hayo, lakini HNC imesisitiza kwamba iwe mwakilishi wa pekee.

Bildergalerie Flüchtlingskinder Situation in Griechenland
Wakimbizi kutoka SyriaPicha: DW/R. Shirmohammadi

HNC imesema kwa lolote lile kuafikiwa ni sharti Rais wa Syria Bashar Al Assad aondoke afisini lakini hayo makundi ya Moscow na Cairo yana msimamo wa kadri kuhusiana na rais Assad.

Huku mazungumzo hayo yakiendelea, mlipuaji wa kujitoa mhanga aliwauwa watu 45 wengi wao waasi, katika mji wa Al-Bab huko Syria, Ijumaa, mji waliokuwa wameuteka kutoka kwa wapiganaji wa kundi la Islamic State IS saa chache kabla tukio hilo.

Taarifa kutoka kwa shirika la kutetea haki za kibinadam la Syria, zilisema mlipuaji huyo alilipua gari lililokuwa limesheheni vilipuzi eneo la Susian, lililoko kilomita nane kaskazini mashariki mwa mji huo wa Al-Bab uliotwaliwa na waasi wanaoungwa mkono na Uturuki siku ya Alhamis, baada ya wiki kadhaa za mapigano.

UNSC kupiga kura wiki ijayo kuhusu silaha za kemikali

Hayo yakiarifiwa, wanadiplomasia wanasema baraza la usalama la Umoja wa Mataifa UNSC mapema wiki ijayo, linatarajiwa kupigia kura azimio litakalowapelekea makamanda na maafisa 11 wa jeshi la Syria kuwekewa vikwazo, kufuatia mashambulizi ya kemikali.

Azimio hilo pia linatarajiwa kuweka marufuku ya kuuzwa kwa ndege aina ya helikopta kwa serikali ya Syria.

Syrien Präsident Bashar al-Assad
Rais wa Syria Bashar Al Assad akataa kutumika kwa silaha za kemikaliPicha: Reuters/SANA

Serikali ya rais Bashar Al Assad imekanusha kwamba wanajeshi wake wametumia zana za kemikali. Kemikali aina ya chlorine inayodaiwa kutumika kama silaha huko Syria, imepigwa marufuku chini ya makubaliano ya zana za kemikali ambayo Syria ilitia saini na kukubali kuyatii mwaka 2013.

Kufuatia uchunguzi uliofanywa na Umoja wa Mataifa, Marekani mwezi Januari iliwawekea vikwazo maafisa 18 wakuu wa Syria iliosema wanahusika na mpango wa silaha za mauaji ya kiasi kikubwa.

Mwandishi: Jacob Safari/AFP/Reuters

Mhariri: Saumu Mwasimba