1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN kupiga kura kuhusu suala la Jerusalem

Bruce Amani
18 Desemba 2017

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litapiga kura leo kuhusu rasimu ya azimio ambalo litapinga uamuzi wa Rais wa Marakeni Donald Trump kuitambua Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel 

https://p.dw.com/p/2pYDc
Jerusalem Proteste nach Freitagsgebet
Picha: Reuters/A. Awad

Misri hapo jana iliomba kupigwa kura hiyo, siku moja baada ya kuwasilishwa azimio hilo ambalo linatazamiwa kupingwa na Marekani kupitia kura ya turufu.

Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence atazuru Jerusalem siku ya Jumatano, akijitumbukiza katika mzozo wa moja kati ya suala lenye utata kabisa katika mzozo kati ya Wapalestina na Israel. Israel ilichukua udhibiti wa sehemu ya mashariki mwa mji  huo  katika vita vya mashariki ya kati mwaka 1967 na inaliona eneo lote la mji  wa Jerusalem kuwa mji ambao haukugawanyika.

Ukraine, mshirika wa Marekani katika baraza la usalama, hata hivyo imeelezea wasiwasi kuhusu uamuzi huo na kuomba kupewa muda wa ziada. Baraza hilo litaandaa kiikao cha faragha leo ili kujadili mswada wa azimio hilo kabla ya kupigiwa kura.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan alielezea matumaini kuwa Uturuki hivi karibuni huenda ikafungua ubalozi katika Jerusalem Mashariki, wakati akilaani kwa mara nyingine hatua ya Trump kuutambua mji huo kuwa mji mkuu wa Israel.

Mswada  huo  wa  azimio  unatoa  wito kwa  nchi  zote kujizuwia kufungua  balozi  zao   mjini  Jerusalem, ukiakisi  wasiwasi  kwamba serikali  nyingine zinaweza  kufuata  kile  Marekani  ilichofanya.

New York UN Botschafter Ägypren Amr Abdellatif Aboulatta
Misri iliwasilisha mswada wa azimio hiloPicha: picture-alliance/Zuma/L. Muzi

Mswada  huo  unataka  kwamba  mataiafa  yote  wanachama kutotambua  hatua  yoyote  ambayo  itakwenda   kinyume  na maazimio  ya  Umoja  wa  Mataifa  kuhusu hadhi ya mji huo. Maazimio kadhaa ya Umoja wa Mataifa yanaitaka Israel kujiondoa kwenye maeneo iliyoyatwaa wakati wa vita yam waka wa 1967 na yanasisitiza kuhusu haja ya kusitisha kukaliwa ardhi hiyo.

Wapalestina walitaka azimio lenye maneno makali ambalo lingeutaka utawala wa Marekani kuufuta uamuzi wake, lakini nakala ya mwisho ilipunguzwa makali ili kutafuta uungwaji mkono wa kutosha.

Huku wakiungwa mkono na nchi za waislamu, Wapalestina wanatarajia kuigekia hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa kuidhinisha azimio linalopinga uamuzi wa Marekani, ikiwa, kama inavyotarajiwa, hatua hiyo itapingwa  na Marekani katika Baraza la Usalama.

Kando na Marekani, Uingereza, China, Ufaransa na Urusi zinaweza kutumia kura a turufu kupinga azimio lolote linalowasilishwa katika baraza hilo, ambalo linahitaji kura tisa ili kuidhinishwa.

Wakati hayo yakijiri, ndege za kijeshi ka Israel zimekishambulia kituo kimoja cha Hamas kaskazini mwa Ukanda wa Gaza mapema leo, saa chache tu baada ya maroketi mawili yaliyofyatuliwa kutokea eneo la Wapalestina kupiga kusini mwa Israel. Wanamgambo katika upande wa Wapalestina  wamekuwa wakifyatua maroketi kuelekea Israel tangu Trump alipotoa tangazo lake lenye utata.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo