1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Ubakaji unatumiwa kama silaha za vita Tigray

16 Aprili 2021

Mkuu wa shughuli za kibinadamu katika Umoja wa Mataifa Mark Lowcock amesema ukatili wa kijinsia na ubakaji unatumiwa kama silaha za vita katika jimbo la kaskazini mwa Ethiopia la Tigray.

https://p.dw.com/p/3s5q3
Bildergalerie Äthiopien | Flucht aus der Region Tigray
Picha: Baz Ratner/REUTERS

Mkuu wa shughuli za kibinadamu katika Umoja wa Mataifa Mark Lowcock amesema ukatili wa kijinsia na ubakaji unatumiwa kama silaha za vita katika jimbo la kaskazini mwa Ethiopia la Tigray, ambapo wasichana wadogo wengine wenye umri wa miaka minane na wanawake wamebakwa.

Lowcock amesema visa vingi vya ubakaji vimefanywa na vikosi vya usalama na kwamba karibu robo ya visa vilivyoripotiwa, vinahusisha ubakaji wa zamu wakati hata wasichana wadogo wenye umri wa miaka minane pia wakilengwa.

Afisa mkuu wa afya katika jimbo hilo, Fasika Amdeselassie, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa kesi 829 za unyanyasaji wa kijinsia zimeripotiwa katika hospitali tano tangu mzozo huo ulipoanza.

Mmoja wa waathiriwa wa ubakaji amesema "Kulikuwa na wanajeshi 23 walionifuata katika sehemu ya jangwani. Wote hao walimbaka mwanamke mmoja, mimi. Wakati nikijaribu kupiga kelele, walibana pumzi zangu."

Äthiopien Konflikte
Picha: Eduardo Soteras/AFP/Getty Images

Lowcock ameliambia baraza la usalama la Umoja wa mataifa kwamba hali ya kibinadamu katika jimbo hilo la kaskazini mwa Ethiopia imezorota katika muda wa mwezi mmoja uliopita.

Soma zaidi: G7 wataka wanajeshi wa Eritrea kuondoka Tigray

Ameongeza kusema kuwa Umoja wa Mataifa haukuona thibitisho lolote kwamba wanajeshi wa Eritrea ambao wanashtumiwa kwa mauaji, wameondoka.

Mkuu huyo wa shughuli za kibinadamu katika Umoja wa mataifa amesema "Nikiwa muwazi kabisa, mzozo katika jimbo la Tigray bado haujakwisha na hali katika jimbo hilo bado haijabadilika." mwisho wa nukuu.

Lowcock amesema usafirishaji wa misaada ya kibinadamu katika jimbo la Tigray umekuwa changamoto, na kwamba amepokea ripoti mapema Alhamisi kuwa watu 150 wamekufa kwa njaa.

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Stepahne Dujarric ametoa wito wa ufikiaji wa misaada ya kibinadamu katika jimbo hilo.

Dujarric amesema katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutterres anaendelea na mazungumzo na wakuu wa serikali za Ethiopia na Eritrea juu ya suala hilo.

"Kwanza ni kuongeza ufikiaji wa misaada ya kibinadamu, kuona harakati za kweli juu ya uchunguzi wa ukiukwaji wa haki za binadamu hasa kufuatia ripoti za kutisha kutoka kwa watu wetu na wakati mwengine ripoti kutoka kwa watu wa serikali ya Ethiopia, na upatanisho wa makundi yanayohasimiana huko Tigray."

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-Greenfield amesema ni wakati baraza la usalama kuzungumza kwa sauti moja juu ya mzozo wa Tigray.

Baraza hilo limeshindwa kuafikiana juu ya suala hilo, wakati nchi za magharibi zikionekana kuwa na mtazamo tofauti na Urusi na China kuhusu jinsi ya kushughulikia mzozo wa Tigray.