1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Watu milioni moja wanakabiliwa na njaa Msumbiji

Bruce Amani
14 Aprili 2021

Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa – WFP limesema karibu watu milioni moja wanakabiliwa na baa la njaa kaskazini mwa Msumbiji, ambako mamia kwa maelfu ya watu wamekimbia kutokana na mashambulizi ya waasi. 

https://p.dw.com/p/3rz3O
Mosambik Flüchtlinge aus Palma in Pemba
Picha: DW

Wanamgambo wa itikadi kali mwezi uliopita wanaohusishwa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu – IS walishambulia Palma, mji mkuu wa mkoa wa Cabo Delgabo karibu na miradi ya gesi inayosimamiwa na kampuni zikiwemo Total na Exxon.

Sasa Shirika la WFP limesema jijini Geneva kuwa watu 950,000 wanakabiliwa na njaa nchini Msumbiji. Shirika hilo la chakula la Umoja wa Mataifa limetoa mwito kwa wafadhili kuchangisha dola milioni 82 ili kuukabili mgogoro huo. Tomson Phiri ni msemaji wa WFP: WFP inapanga kuwasaidia karibu watu 750,000 waliopoteza makaazi na jamii zinazoishi katika mazingira magumu mkoani Cabo Delgado na mikoa jirani ya Nampula, Niassa na Zambezia.

Naye mkurugenzi mkuu wa masuala ya dharura wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia Watoto – UNICEF Manuel Fontaine, aliuambia mkutano huo wa waandishi wa habari kuwa mashirika hayo yanakabiliwa na hali ngumu ya kibinaadamu na ambayo huenda ikadumu kwa muda mrefu.

Mosambik Flüchtlinge aus Palma in Pemba
Wakimbizi wanaishi katika kambi za muda Cabo DelgaboPicha: DW

Kuna simulizi za watu kutekwa, za dhulma za kijinsia, simulizi za kutisha za watu hawa wote kufanya kazi kwa siku nyingi, watoto wanaowasili na miguu iliyovimba na wakiwa wameumia, na kuhitaji kuhudumiwa.

Soma zaidi: Wakuu wa SADC walaani uasi nchini Msumbiji

Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamiaji – IOM limesema karibu watu 690,000 walikuwa tayari wamepoteza makaazi yao kote nchini humo kufikia Februari. Wengine 16,500 wamesajiliwa katika maeneo menfine ya Cabo Delgado baada ya kukimbia makwao kufuatia shambulizi la Palma.

Wengi walikimbilia Kijiji kilicho karibu cha Quitunda, kilichojengwa na kampuni kubwa ya nishati ya Ufaransa Total ili kuwahifadhi waliopoteza makaazi kufuatia mradi wake wa gesi wa kiasi cha bilioni 20. Total iliwaondoa wafanyakazi wake katika eneo hilo kutokana na harakati za uasi mnamo Aprili 2.

Kituo cha Uadilifu wa Umma nchini Msumbiji kinasema serikali imeshindwa kuushughulikia mzozo huo, huku ikiyategemea Zaidi mashirika ya misaada kuwasaidia wale wanaokimbia machafuko. Wengi walibaki katika maeneo ya vita kwa sababu hawana mbinu za kufika maeneo salama.

Reuters