1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaadhimisha miaka 70 ya ulinzi wa amani duniani

Mohammed Abdulrahman
29 Mei 2018

Mei 29 ni siku ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa. Mwaka huu wa 2018 imetimia miaka 70 ya "huduma na kujitolea mhanga."

https://p.dw.com/p/2yUqa
Südsudan UN-Blauhelme aus Ruanda
Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Rwanda, wakiwa kazini nchini Sudan Kusini, ambako mgogoro unaendelea tangu mwaka 2013.Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Lynch

Ni nafasi ya  kukumbuka mchango wa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa na  raia watumishi wa  taasisi hiyo zaidi ya  3,700 waliopoteza maisha yao wakiitumikia bendera ya Umoja wa Mataifa tokea 1948, wakiwemo 129 waliouwawa mwaka jana  2017.

Siku hii inasherehekewa wakati Umoja wa Mataifa ukiwa ni chombo cha pekee cha kuendeleza na kuzisaidia nchi zilizoharibiwa  kutokana na migogoro na badala yake kuweka mazingira  ya kuleta amani ya kudumu katika nchi hizo.

Shughuli za kwanza za kulinda  amani zilianzishwa  Mei 29  1948, pale  Baraza la Usalama lilipoamuru kutumwa kikos kidogo cha wangalizi wa kijeshi wa Umoja wa Mataifa katika Mashariki ya Kati, kuunda kile kilichojulikana  kama  Kikundi cha kusimamia usitishaji mapigano (UNTSO) kufuatia makubaliano ya kusitisha matumizi ya silaha yaliofikiwa baina  ya Israel na mataifa  jirani ya Kiarabu.

Elfenbeinküste UN Einsatz
Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa waliotumwa nchini Cote di'Voire kusimamia usalimishaji wa silaha na wapiganaji wa zamani katika wilaya ya Abobo mwaka 2012.Picha: picture alliance/dpaPANAPRESS/MAXPP/G. Barnus

Kwa zaidi ya miongo saba, zaidi ya  watu milioni moja  wanaume na wanawake wamekuwa wakitumika chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa katika shughuli 71 za kulinda amani, huku moja kwa moja wakihusika katika kuwahudumia  mamilioni ya watu na kulinda maisha yao.

Huduma ya kujitoa mhanga

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanajitolea muhanga  na mara nyingi katika maeneo ya hatari na katika mazingira magumu. Muhanga huu pia  ni wa familia za wale  wanaotoa huduma hizo pamoja na serikali zao.

Kuanzia Sierra Leone hadi jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo , Cambodia, Namibia, El Salvador na kwengineko, askari wa kulinda amani wamesaidia  nchi husika kuweza kujitoa kutoka kwenye vita na kuwa na amani.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Liberia (UNMIL) ulifanikiwa kumaliza shughuli zake mwezi Machi mwaka huu, ukiwa ni ujumbe wa 57 wa shughuli za kusimamia amani za Umoja wa Mataifa kufanya hivyo.

Leo hii Umoja wa Mataifa  una zaidi ya  wanajeshi 100,000, polis na watumishi wa kiraia  katika  jumbe 14 za kulinda amani katika mabara manne.

Ushirikiano katika kulinda amani

Kwa wakati huu  mataifa 124 wanachama yamechangia wanajeshi na  polisi pamoja na vifaa muhimu katika harakati za kulinda amani.

Mali UN-Mission MINUSMA
Picha hii inaonyesha helikopta mbili aina ya Caiman zikipakiwa kwenye ndege ya mizigo Februari 15, 2018, tayari kusafirishwa nchini Mali kujiunga na ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSMA. Picha: Imago/Belga

Harakati za kusimamia amani ni ushirikiano wa kimataifa na idadi hiyo inaashiria kujizatiti na kujitoa kwa wanacahama wake katika lengo hilo.

Wakati siku ya  kulinda amani ya Umoja wa Mataifa ni Mei 29, Umoja wa Mataifa utasherehekea siku hii mwaka huu hapo Juni mosi kwenye makao yake makuu mjini New York .

Sambamba na hayo Umoja huo utakabidhi Medali ya Dag Hammarskjöld kwa  walinda amani waliokufa  mwaka 2017 wakiwa katika jukumu  na utumishi wao wa kusimamia amani.

Barani Afrika mbali ni pamoja na jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ukiwa ujumbe mkubwa kabisa  duniani  na pia jamhuri ya Afrika Kati.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman

Mhariri: Iddi Ssessanga