1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaionya Taliban kuhusu haki za wanawake na wasichana

22 Juni 2023

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afghanistan amewatahadharisha watawala wa Taliban kwamba itakuwa vigumu kupata uhalali wa kimataifa iwapo wataendeleza ukandamizaji wa haki za wanawake na wasichana.

https://p.dw.com/p/4SvT7
Afghanistan Frauen-Rechte | Demo in Berlin
Picha: Olaf Schuelke/IMAGO

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afghanistan Roza Otunbayeva amewatahadharisha watawala wa kundi la Taliban kwamba itakuwa vigumu kupata uhalali wa kimataifa iwapo wataendeleza ukandamizaji wa haki za wanawake na wasichana.

Mwanadiplomasia huyo alikuwa akizungumza mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York akitoa tathmini ya hali nchini Afghanistan.

Soma pia: Mateso ya Taliban kwa wanawake ni uhalifu dhidi ya ubinadamu

Bibi Roza amewaarifu watawala wa Taliban katika moja ya mazungumzo aliyofanya na kundi hilo, kwamba hawataweza kuvutia uungaji mkono wa kimataifa hadi watakapoondoa vizuizi walivyoweka dhidi ya haki ya wanawake na wasichana kupata elimu pamoja na kufanya kazi.

Tangu lilipochukua madaraka nchini Afghanistan mnamo mwaka 2021 kundi la Taliban limelaumiwa kwa kuweka vizuizi vikali kwa wanawake kupata elimu au kufanya kazi.