1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yamnyooshea kidole Assad mauaji ya Treimsa

14 Julai 2012

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa na jumuiya ya nchi za kiarabu kwenye mgogoro wa Syria, Koffi Annan ameilaumu serikali ya rais Bashar al-Assad kwa kutumia silaha nzito dhidi ya kijiji cha wakulima cha Treimsa.

https://p.dw.com/p/15Xh3
Roketi ya Syria.
Roketi ya Syria.Picha: picture-alliance/dpa

Umoja wa Mataifa umeinyooshea kidole serikali ya Assad, kwa mauaji ya kutisha yaliyofanyika katika kijiji hicho, katika hatua ambayo inazua maswali juu ya ufanisi wa diplomasia katika mgogoro huo uliyodumu kwa miezi 16 sasa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua kukomesha unyama huo.

Wakati mgogoro huo unazidi kuchukua sura ya kinyama zaidi, wachambuzi wanaonya kuwa juhudi za mjumbe maalumu Annan, zimetumbukia nyongo. Ban na Annan wamechukizwa na mauaji ya siku ya Ijumaa, ambapo kiasi ya watu 200 wanasemakana kuuawa, na wametaka shinikizo liongezwe kwa rais Bashar Assad, ambaye utawala wake ulianzisha ukandamizaji dhidi ya waandamanaji waliyokuwa wanadai demokrasia.

Maandamano dhidi ya utawala wa Bashar al-Assad.
Maandamano dhidi ya utawala wa Bashar al-Assad.Picha: picture-alliance/dpa

"Natoa wito kwa mataifa wanachama kuchukua hatua za pamoja ili kuzuia janga linaloinyemelea Syria. Kutochukuwa hatua ni kutoa leseni kwa mauaji mengine," alisema Ban katika taarifa iliyojaa hisia na aliyoielekeza kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Mauaji ya Treimsa yameongeza dharura katika mazungumzo yaliyokwama kuhusiana na azimio la Baraza la Usalama juu ya mgogoro wa Syria.

Urusi yaendeleza msimamo wake wa kupinga
Urusi imeendelea kupinga hatua zozote za kuiwekea Syria vikwazo visivyo vya kijeshi ili kuilaazimisha kutekeleza mpango wa amani uliyopendekezwa na Koffi Annan. Marekani imetaka kusitishwa kwa mapigano ili kupisha waangalizi wa Umoja wa Mataifa kuingia kijiji cha Treimsa kilichopo katika mkoa wa kati wa Hama.

Annan alisema matumizi ya silaha kubwa, vifaru na helikopta za kivita, ambavyo vimethibitishwa na timu ya waangalizi ya Umoja wa Mataifa, ni ukiukaji wa serikali ya Syria, kutekeleza wajibu wake na ahadi ya kuacha kutumia zana nzito katika maeneo ya raia. "Cha kusikitisha ni kwamba tuna ukumbusho mwingine kwamba maazimio ya Baraza yanaendelea kukiukwa," alisema Annan.

Wapinzani wa Baraza la Taifa la Syria, Abdelbasset Sida, (k) na Goerge Sabra wakati wa mkutanno na waandishi wa habari mjini Istandul, Uturuki, Ijumaa.
Wapinzani wa Baraza la Taifa la Syria, Abdelbasset Sida, (k) na Goerge Sabra wakati wa mkutanno na waandishi wa habari mjini Istandul, Uturuki, Ijumaa.Picha: Reuters

Idadi sahihi ya watu wliouawa katika tukio hilo haijafahamika vizuri. Ijumaa jioni wanaharakati walipunguza idadi ya awali ya zaidi ya watu 200. Moja alisema walithibitisha watu 74 lakini alikuwa na majina 20 tu. Mwingine alitoa majina ya watu 103. Kwa upande wake, serikali ya Syria ilisema watu 50 waliuawa wakati majeshi yake yalipopambana na makundi yaliyokuwa yanawafanyia ugaidi wakaazi wa kijiji hicho. Utawala huo unatumia majina ya 'magaidi na majambazi' kuwaelezea wapinzani wake.

Mauaji bado yagubikwa na utata
Haijafamika wazi ni nini hasa kilichotokea katika kijiji cha Treimsa, ambacho kimejitenga katika mkoa wa Hama, ikiwa ni pamoja na nini kilisababisha kulengwa kwake na kama wote waliouwa walikuwa raia. Kundi moja la wanaharakati lilisema waathirika kadhaa wa mashambulizi hayo walikuwa wapiganaji wa waasi.

Picha moja ya video iliyowekwa kwenye mtandao, ilimuonyesha kijana mdogo akilia mbele ya mwili wa mwanaume mmoja mzee uliozungushwa katika blanketi. Picha nyengine ilionyesha kaburi lenye upana wa maiti tatu na urefu wa maiti kumi, huku msimulizi akiliita la kwanza la kundi la mashahidi wa mauaji ya Treimsa.

Waangalizi wa amani wathibitisha matumizi ya silaha nzito
Kiongozi wa timu ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa, Meja Jenerali Robert Mood aliwaambia waandishi wa habari mjini Damascus kuwa kundi la waangalizi lililowekwa kilomita tatu kutoka Treimsa lilitibitisha matumizi ya zana nzito za kivita na helikopta, jambo linaloitia hatiani serikali.

Moshi ukitanda anagani kufuatia mashmbulizi katika mji wa Homs.
Moshi ukitanda anagani kufuatia mashmbulizi katika mji wa Homs.Picha: AP

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton, siku ya Ijumaa alilaani mauaji ya Treimsa na kulitaka Baraza la Usalama kuchukua hatua kukomesha umuagaji damu. "Historia italihukumu Baraza hili," alisema Clinton na kuongeza kuwa wanachama wake wanapaswa kujiuliza endapo kuendelea kuuacha utawala wa Assad ufanye unyama dhidi ya raia wake ndiyo kumbukumbu linalotaka kuacha.

Kwa upande wake, Urusi ililaani mauaji ya Treimsa lakini iliyalaumu kwa wapinzani wa rais Assad. Utawala wa Assad unadai uasi huo ni njama ya mataifa ya nje kuidhoofisha Syria, huku ikiwachukulia wapinzani nchini humo, kuanzia waandamanaji wanaodai demokrasia hadi waasi kama magaidi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE, AP
Mhariri: Sekione Kitojo