1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yampeleka afisa wa shughuli za amani nchini Afghanistan

Kabogo Grace Patricia23 Oktoba 2009

Afisa huyo, Wolfgang Weisbrod-Weber anachukua nafasi ya Peter Galbraith, aliyefukuzwa kazi.

https://p.dw.com/p/KDaW
Peter Galbraith, ambaye nafasi yake imezibwa na Wolfgang Weisbrod-Weber.Picha: AP

Umoja wa Mataifa umempeleka Afghanistan afisa wa Kijerumani wa shughuli za kusimamia amani, Wolfgang Weisbrod-Weber, kuwa kaibu naibu wa Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini humo Bw Kei Eide, kwa muda wa miezi miwili ijayo. Msaidizi wa zamani wa Bwana Eide, Mwanadiplomasia wa Marekani Peter Galbraith, alifukuzwa kazi baada ya kutokubaliana wazi wazi na jinsi Umoja wa Mataifa ulivyokuwa ukifatilia uchaguzi wa Agosti 20, mwaka huu nchini Afghanistan.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Marie Okabe amesema katika wakati huu wa matatizo kuelekea duru ya pili ya uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 7 mwezi ujao wa Novemba, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon ameamua kumpeleka kwa muda mwanadiplomasia Weisbrod-Weber nchini Afghanistan kufanya kazi na Eide msaidizi wake wa masuala ya kisiasa. Uchaguzi huo wa duru ya pili utafanyika baada ya Rais aliyeko madarakani, Hamid Karzai kushindwa kupata asilimia 50 ya kura inayohitajika kwa mgombea kushinda. Katika uchaguzi huo, Rais Karzai atakabiliana na mpinzani wake mkuu, Abdullah Abdullah, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Afghanistan. Weisbrod-Weber ni mkurugenzi wa idara ya Asia na Mashariki ya Kati katika kitengo cha majeshi ya kulinda amani kwenye makao makuu wa Umoja wa Mataifa huko New York.

Hali ya usalama

Wakati hayo yakijiri, afisa wa juu wa Afghanistan amesema nchi hiyo haitakuwa na muda wa kutosha kwa ajili ya kuhakikisha usalama unakuwepo wakati wa duru ya pili ya uchaguzi wa rais. Huku vurugu zikiendelea Afghanistan, duru hiyo ya pili ya uchaguzi inafanyika wakati Rais Barack Obama wa Marekani anapima endapo apeleke wanajeshi zaidi nchini humo kwa ajili ya kukabiliana na wanamgambo wa Taliban. Wasi wasi kuhusu hali ya usalama na kurudiwa kwa udanganyifu uliotokea katika duru ya kwanza ya uchaguzi tayari vimekuwa doa baada ya wiki kadhaa za mashaka kisiasa. Daoud Ali Najafi, afisa mkuu wa uchaguzi katika Tume Huru ya Uchaguzi iliyoteuliwa na serikali amesema ana wasi wasi kama vikosi vya usalama vitaweza kuhakikisha kuwa vituo vya kupigia kura vinakuwa salama kwa ajili ya wapiga kura. Matukio kadhaa ya mashambulio ya mabomu wakati wa duru ya kwanza ya uchaguzi yalisababisha wananchi wengi wa Afghanistan kutokwenda kupiga kura, ingawa kundi la Taliban lililoahidi kuvuruga uchaguzi huo kutofanikiwa kufanya hivyo kwa kiasi kikubwa.

Hatua za haraka za kuchukua

Taasisi ya kimataifa ya Republican, ambayo waangalizi wake walifuatilia uchaguzi wa mwezi Agosti, wameitaka Afghanistan na washirika wake wa kigeni kuchukua hatua za haraka kuhakikisha usalama unakuwepo wakati wa uchaguzi. Katika taarifa yake taasisi hiyo imesema Afghanistan inakabiliwa na changamoto kadhaa katika maandalizi yake ya duru ya pili ya uchaguzi. Najafi amesema ameshafanya mazungumzo na Jumuiya ya Kujihami ya NATO na mawaziri wa ulinzi na mambo ya ndani wa Afghanistan na tayari amewasilisha idadi ya vituo vya kupigia kura ambavyo hali ya usalama inabidi iimarishwe kwanza kabla ya siku ya kupiga kura.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/RTRE)

Mhariri: M.Abdul-Rahman