1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yataka kuundwa chombo kuichunguza Myanmar

Lilian Mtono
10 Septemba 2018

Mkuu wa Shirika la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ametaka kuundwa kwa jopo litakalopewa jukumu la kuandaa mashitaka juu ya mauaji ya kiholela yaliyofanywa nchini Myanmar.

https://p.dw.com/p/34bgT
Michelle Bachelet
Picha: picture-alliance/dpa/S. Wenig

Mkuu wa Shirika la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ametaka kuundwa kwa jopo litakalopewa jukumu la kuandaa mashitaka juu ya mauaji ya kiholela yaliyofanywa nchini Myanmar, katika wakati ambapo kuna madai ya mauaji ya halaiki dhidi ya jamii ya Waislamu walio wachache ya Rohingya. 

Kwenye hotuba yake ya kwanza kama mkuu  haki za binaadamu kwenye Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ametoa mwito kwa baraza hilo kuunda chombo huru cha kimataifa kitakachokusanya, kuhifadhi na kuchambua ushahidi wa uhalifu mbaya kabisa wa kimataifa, ili kuharakisha mashitaka huru na ya haki katika mahakama za kitaifa na kimataifa. Chombo kama hicho tayari kimeundwa kwa ajili ya mzozo wa Syria.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa, mwezi uliopita ulichapisha ripoti ya uharibifu, iliyotimisha kwamba kulikuwa na ushahidi wa kutosha wa kuwafungulia mashitaka ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu na mauaji ya halaiki dhidi ya Warohingya, maafisa wa kijeshi wa Myanmar pamoja na makamanda wengine watano waandamizi wa jeshi.

Bachelet ambaye ni rais wa zamani wa Chile, amesisitiza kwamba jopo hilo pia litaunga mkono na kusaidia uchunguzi wa awali wa mwendesha mashitaka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC.

Bangladesch Rohingya Flüchtlinge in Kutupalong Flüchtlingslager
Wakimbizi wa Myanmar waliokimbia Rakhine na kwenda Bangladesh.Picha: picture-alliance/NurPhoto/T. Chowdhury

Takriban Warohingya 700,000 walikimbilia Bangladesh wakitokea jimbo la kaskazini la Rakhine, kufuatia Myanmar kuanzisha hatua kali na za kikatili dhidi ya waasi mwezi Agosti mwaka jana.

Kuhusu uhamiaji, Bachelet amesema juhudi za serikali za kuwarejesha raia wa kigeni, hazitasaidia katika upatikanaji wa suluhu ya mzozo wa uhamiaji, na badala yake ni chanzo cha uadui mpya.

Amesema, ni kwa maslahi ya kila taifa kuwa na sera za uhamiaji zinazozingatia uhalisia.

Bachelet amekosoa hatua za kujenga kuta za mipaka, kutenganisha familia za wahamiaji na uchokozi utakaozusha ghadhabu kwa wahamiaji. Amesema, sera kama hizo hazitoi suluhu ya muda mrefu kwa yeyote, na zaidi husababisha uadui, mateso, taabu na machafuko.

Frankreich - Polizei räumt Flüchlingscamp bei Dünkirchen
Baadhi ya wahamiaji waliofukuzwa kwenye kambi Picha: Getty Images/AFP/P. Huguen

Ingawa hakurejelea mfano mahsusi kwenye matamshi yake, lakini ameyataja mataifa kama Marekani, Hungary na Italia katika toleo refu la hotuba hiyo lililowasilishwa kwa baraza.

Aidha amesema, atatuma timu nchini Australia na Italia kuangazia namna ya kuwalinda wahamiaji, huku akielezea wasiwasi wake kuhusu watoto 500 wahamiaji waliopo nchini Marekani, waliotenganishwa na wazazi wao na ambao bado hawajarejeshwa makwao.

Katika hatua nyingine, Bachelet ameitaka China kuwaruhusu wachunguzi kuingia nchini humo, kufuatia kile aichoita ni "madai yenye kuchukiza sana” kuhusu makambi makubwa ambamo Jamii ya Waislamu walio wachache ya Uighur na wanaokabiliwa na hatua kali kutoka kwa serikali ya China, wanashikiliwa.

Kuhusu mzozo wa Yemen, Bachelet ameutaka muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia kuonyesha uwazi zaidi katika kanuni zake za kivita na kuwafungulia mashitaka wahalifu waliofanya mashambulizi ya angani dhidi ya raia, hususan shambulizi la basi lililokuwa limebeba watoto katika mji wa Saada mwezi uliopita.

Michelle Bachelet ameanza rasmi kutekeleza majukumu yake mwanzoni mwa mwezi huu, akichukua madaraka kutoka kwa mwanadilpomasia wa Umoja wa Mataifa, Zeid Raad Al-Hussein.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/RTRE/AFPE.

Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman