1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNFPA-Mamilioni ya wanawake hawana maamuzi na miili yao

Saumu Mwasimba
14 Aprili 2021

Wanawake na wasichana wengi wananyimwa uhuru wa kujiamualia juu ya kutumia njia za kupanga uzazi,au huduma za kutoa mimba,wanalazimishwa kupitia ukeketaji na hata kufanyiwa uchunguzi wa bikra zao.

https://p.dw.com/p/3rzTt
EcoAfrica Sendung 13.11.2020
Picha: DW

((Mamilioni ya wanawake duniani wananyimwa uhuru wa kufanya maamuzi juu ya miili yao wenyewe. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyochapishwa leo.

Taarifa kutoka nchi 57 nyingi zikiwa za kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika zinaonesha kwamba ni nusu tu ya wasichana waliokwisha balekhe na wanawake ndio wana fursa ya kujifanyia maamuzi binafsi,kuhusu miili yao na uhuru kwa ujumla wa kuamua chochote. Hapa uhuru unaozungumziwa unajumuisha pia masuala kama hatua ya mwanamke kujichagulia binafsi ni nani wa kufanya nae mapenzi,au kutumia njia za mpango wa uzazi.

Hii ni ripoti iliyochapishwa na shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na idadi ya watu UNFPA. Mkuu wa shirika hilo Natalia Kanem ameitaja hali hiyo kuwa ya kushtusha sana.Kwa mujibu wa Kanem ripoti hiyo ni ya kushtusha kwasababu mamia ya mailioni ya wanawake na wasichana sio wamiliki wa miili yao wenyewe na maisha yao yanafanyiwa maamuzi na watu wengine.

Natalia Kanem
Picha: Luiz Rampelotto/EuropaNewswire/picture alliance

Katika ripoti hii pia mkuu huyo wa UNFPA ametaja kwamba hali ya wanawake wengi imezidi kuwa mbaya kutokana na janga la virusi vya Corona.Akitolea mfano amesema hivi sasa rikodi ni kubwa zinazoonesha idadi ya wanawake na wasichana walioko kwenye hatari ya kukabiliwa na unyanyasaji wa kijinsia  na vitendo vya madhara kama ndoa za utotoni. Kutokana na hali hii Kanem ameitolea mwito Jumuiya ya Kimataifa kujitowa zaidi katika suala la usawa wa kijinsia.

 Ukweli wa mambo ni kwamba licha ya kuwepo ahadi za kikatiba za kushughulikiwa usawa wa kijinsia katika nchi nyingi,kwa wastani wanawake wanafursa ya kufurahia asilimia 75 tu ya haki zao za kisheria ikilinganishwa na wanaume.Na hayo yamebainika kupitia takwimu za mwaka 2020 zilizotajwa na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Imeelezwa kwenye ripoti hii kwamba wanawake katika nchi za Afrika,Kusini mwa Jangwa la Sahara,Asia ya Kati na Kusini ndio wenye nafasi ndogo sana ya uwezekano wa kuihodhi miili yao na kufikia umbali wa kukataa kufanya mapenzi na wenzawao au kupata huduma ya afya ya uzazi bila ya kuhitaji ridhaa ya mmwenza wake au jamaa yake wa kiume.

Ripoti hapa imetowa mfano wa Mali,Niger na Senegal ambako ni asilimia 10 tu ya wanawake ndio wenye mamlaka na miili yao. Wanawake na wasichana wengi wananyimwa uhuru wa kujiamualia juu ya kutumia njia za kupanga uzazi,au huduma za kutoa mimba,wanalazimishwa kupitia ukeketaji na hata kufanyiwa uchunguzi wa bikra zao wakati wengine wakiozwa katika umri mdogo.

Na kwa kukamilisha ripoti hii inasema kwamba wanawake na wasichana mara nyingi wanalazimishwa kuwaachia wengine kuwafanyia maamuzi juu ya miili yao na watafiti pia wanatabiri kwamba ndoa milioni 13 za ziada za  watoto wadogo na visa milioni 2 vingine vya ukeketaji huenda vikashuhudiwa katika kipindi kingine cha muongo mmoja,wakati janga lililopo likiendelea kuzibana juhudi za kumaliza vitendo hivyo.

Source:Reuters/dpa