1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

UN:India kuipiku China kwa idadi ya watu

Angela Mdungu
19 Aprili 2023

Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu limesema kuwa India inatarajiwa kuchukua nafasi ya kwanza kwa idadi ya watu duniani ifikapo katikati mwa mwaka huu.

https://p.dw.com/p/4QIOc
Indien | Weltbevölkerung
Picha: Kabir Jhangiani/ZUMA Press/picture alliance

 Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu, UNFPA iliyochapishwa leo, ambapo hatua hiyo itaifanya India kuiondoa China kwenye nafasi hiyo ya kwanza ikiizidi kwa tofauti ya watu milioni 3.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo India itakuwa na wakaazi bilioni 1.4286, wakati China ikiwa na watu bilioni 1.4257. Mbali na India na China, ripoti hiyo ya UNFPA imekadiria kuwa idadi jumla ya watu dunia itafikia bilioni 8.045. Umoja wa Mataifa umesema kuwa kutokana na taarifa zilizotolewa, hakuna uwezekano wa kujua ni siku gani hasa India itaipiku China.

Kwa mara ya mwisho, India ilifanya sensa mwaka 2011. Sensa mpya ilitakiwa kufanyika mwaka 2021 lakini iliahirishwa. Ongezeko la watu kati ka mataifa hayo mawili imekuwa ikishuka katika kipindi cha hivi karibuni.

Soma zaidi:Idadi ya watu kufikia bil.8 ifikapo Novemba

 Idadi ya watu kwa upande wa China ilipungua mwaka uliopita ikiwa ni mara ya kwanza ndani ya miongo sita. Kwa sasa, idadi ya watu kwa upande wa India inatarajiwa kuendelea kukua.

Haki za uzazi za wanawake zizingatiwe zaidi

Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa hii leo limeitaka dunia kuangazia zaidi haki za  wanawake katika masuala ya uzazi ili kuimarisha uelewa na matarajio ya mienendo ya idadi ya watu, badala ya kuangalia athari za ongezeko la watu duniani.

Shirika la UNFPA linatambua kuwa kulikuwa na shauku kubwa juu ya ukubwa wa idadi ya watu duniani inayotarajiwa kufikia bilioni 10.04 Itakapofika miaka ya 2080. Limesema mkazo unapaswa kuwekwa katika kuwapa wanawake nguvu ya kuamua ni lini na nivipi wangependa kuwa na watoto.

Mkuu wa shirika hilo Natalia Kanem amesema asilimia 44, karibu na nusu ya idadi ya wanawake wanashindwa kuamua kuhusu miili yao ikiwemo kufanya maamuzi kuhusu njia za mpango wa uzazi, huduma za afya. Amesema karibu nusu ya mimba zinazotungwa nuniani kote hazikukusudiwa.

Kanem ameongeza kuwa nchi zenye kiwango kikubwa cha uwezo wa kuzaa zinachangia pakubwa ongezeko la joto duniani na ndizo zinazopata madhara zaidi.

Mkurugenzi mtendaji wa UNFPA
Mkurugenzi mtendaji wa UNFPAPicha: Luiz Rampelotto/EuropaNewswire/picture alliance

Mkuu huyo wa shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu UNFPA ameongeza kwamba, nafasi ya nchi katika faharasa ya mataifa yenye watu wengi zaidi itabadilika kwa kiasi kikubwa katika miaka 25 ijayo.

Mataifa nane yanatarayiwa kuwa yatachangia nusu ya makadirio ya ukuaji wa idadi ya watu duniani ifikapo mwaka 2050. Mataifa hayo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Misri, Ethiopia, India, Nigeria, Pakistani, Ufilipino na Tanzania.