1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNRW yakabiliwa na mzozo wa fedha

Lilian Mtono
15 Machi 2018

Mataifa makubwa duniani yanakutana mjini Rome kujadili hatima ya shirika la kuhudumia wakimbizi la Palestina, UNRWA linalokabiliwa na mzozo mkubwa wa kifedha baada ya Marekani kusimamisha mamilioni ya dola ya ufadhili. 

https://p.dw.com/p/2uM7k
Israel - Palästina | Symbolbild UNWRA
Picha: Getty Images/AFP/M. Hams

Mataifa makubwa duniani yanakutana mjini Rome hii leo kujadiliana juu ya mustakabali wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Palestina, UNRWA linalokabiliwa na mzozo mkubwa wa kifedha baada ya Marekani kusimamisha mamilioni ya dola ya ufadhili wa shirika hilo. 

Kamishna wa UNRWA, Pierre Krahenbuhl, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, shirika hilo la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina  limebakiwa na fedha zitakazojitosheleza kwa ajili ya kusaidia shule na huduma za tiba hadi mwezi Mei.

Serikali ya Marekani chini ya rais Donald Trump hadi sasa imeahidi kiasi cha dola milioni 60 kusaidia shirika hilo mwaka huu, kiasi ambacho ni pungufu kutoka dola milioni 360 zilizotolewa mwaka 2017. 

Trump amesitisha mafungu mawili ya zaidi ya dola milioni 100, moja lililopangiwa kwa ajili ya kusaidia bajeti kuu ya shirika hilo la UNRWA na jingine kwa ajili ya misaada ya chakula.

Mapema mwezi uliopita kwenye kikao cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, rais wa Palestina Mahmoud Abbas aliikosoa hatua hiyo ya Marekani ya kusimamisha misaada, na kusisitiza kuwa iwapo wataendelea na msimamo huo, watarajie kuibuka kwa mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi ama ugaidi.

USA | Trump in Pennsylvania
Serikali ya rais Donald Trump imeahidi dola milioni 60 tu hadi sasaPicha: picture-alliance/dpa/AP/C. Kaster

Trump ameendelea kuwashinikiza viongozi wa Palestina kumaliza mgomo wao dhidi ya serikali yake, kufuatia hatua yake ya mwezi Disemba ya kuitambua Jerusalem kuwa ni mji mkuu wa Israel.

Ni kiwango kidogo tu cha fedha kimepatikana kupitia mkakati mkubwa uliozinduliwa na UNRWA wa kukusanya fedha baada ya Marekani kusimamisha ufadhili, na wanadiplomasia hawana matumaini ya kutolewa ahadi kubwa za fedha kwenye mkutano huo wa Rome.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanayataka mataifa ya Umoja wa Ulaya kujaza pengo lililobaki, lakini kwa wakati huu wanaangazia zaidi mataifa ya Kiarabu kukusanya fedha hizo.

Hata hivyo wasiwasi unazidi kuongezeka kuhusu hatima ya shirika hilo, lililoajiri zaidi ya watumishi 20,000 na wengi miongoni mwao wakiwa ni raia wa Palestina na ambalo limeitegemea zaidi Marekani kwa takriban asilimia 30 ya bajeti yake.

Syrien Flüchtlingsviertel Jarmuk in Damaskus
Baadhi ya wakimbizi wakiwa wanasubiri msaada wa chakula kutoka UNRWAPicha: Getty Images/United Nation Relief and Works Agency

Shirika hilo linatoa msaada mkubwa kwa wakimbizi wa Kipalstina walioko Syria, Lebanon, Jordan, Ukingo wa Magharibi na Gaza, na linawafikia zaidi ya watu milioni tatu.  

Mnamo mwezi Januari, Trump aliandika kupitia ukurasa wake wa twitter kwamba na hapa namnukuu "tunawalipa Wapalestina mamia kwa mamilioni ya dola kwa mwaka na lakini hatupati shukrani wala heshima" mwisho wa kumnukuu, na kuwatuhumu kwa kukataa mazungumzo ya amani.

Wiki mbili baadae serikali yake ilithibitisha kuwa itasitisha makumi kwa mamilioni ya ufadhili kwenye shirika hilo la misaada, ikisema ilitaka mataifa mengine kulipa zaidi. Krahenbul aliitaja hatua hiyo kuwa ni mzozo mbaya zaidi kuwahi kutokea kwenye shirika hilo na kuzindua mkakati wa kukusanya fedha.

Mkutano wa Rome, unaoandaliwa kwa ushirkiano na Sweden, Misri na Jordan utajaribu kuweka hamasa mpya ya kutoa michango kwa shirika hilo. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres atahudhuria, ofisi yake imethibitisha juzi Jumanne.

Balozi wa Sweden kwenye Umoja wa Mataifa, Olof Skoog amesema ilikuwa ni busara kwa dunia kuwajibika zaidi kwa ajili ya UNRWA.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE.

Mhariri:  Daniel Gakuba